Nora Damian, Dar es Salaam
Wabunge watano wanatarajia kufungua kesi ya kikatiba kuiomba Mahakama Kuu ya Tanzania kutoa tafsiri ya kisheria juu ya mipaka ya kinga ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mamlaka ya Spika wa Bunge.
Wabunge hao ni Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), Salome Makamba (Viti Maalumu), Hamidu Bobali (Mchinga), Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini).
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Zitto amesema wamemuagiza Wakili wao Fatma Karume kuisajili kesi hiyo chini ya hati ya dharura.
“Tunaiomba mahakama iitazame kesi hii kwa muktadha mpana kwani ina maslahi makubwa kwa umma.
“Tukiacha CAG aitwe na aende madhara yake ni kwamba iko siku ataitwa jaji mkuu je, kutakuwa na uhuru wa mahakama?” amehoji Zitto.
Hivi karibuni, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimuagiza CAG, Profesa Mussa Assad kuripoti kwenye Kamati ya Kinga na Maadili ya Bunge, kuhojiwa kwa madai ya kulidhalilisha Bunge.