KINSHASA, Congo DRC
TUME ya Uchaguzi nchini hapa imechelewesha kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais, huku kukiwa na ongezeko la shinikizo kutoka mataifa yenye nguvu na Kanisa Katoliki kuheshimu matakwa ya wapiga kura.
Mkuu wa tume hiyo, CENI aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP, kwamba matokeo ya awali, ambayo yalipangwa kutolewa jana sasa yatatolewa wiki ijayo masaa machache kabla ya muda wa mwisho kumalizika.
“Haitawezekana kutangaza matokeo siku ya leo (jana). Tunapinga hatua, lakini hatuna kila kitu bado,” alisema Corneille Nangaa bila ya kueleza siku ya kutangaza matokeo hayo.
Baraza la maaskofu wa Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini hapa , CENCO, ambalo linawakilisha maaskofu wa kikatoliki nchini kote , limeonya kwamba hasira za umma zinaweza kujitokeza iwapo matokeo ya mwisho hayatakuwa ya kweli kwa mujibu wa matokeo halisi ya kura.
Kanisa katoliki lenye ushawishi nchini, ambalo limetoa zaidi ya wachunguzi 40,000 , lilisema mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba linamjua mshindi wa uchaguzi huo, lakini halikumtaja.
Katika barua iliyotumwa kwa Nangaa juzi, Rais wa Baraza la CENCO, Marcel Utembi alisema kutokana na ucheleweshaji huo, iwapo kutakuwa na vuguvugu la maandamano ya umma litakuwa ni jukumu la CENI.
Uchaguzi huo wa Desemba 30 ulishuhudia wagombea 21 wakipambana kuwania kuchukua nafasi ya Rais Joseph Kabila, ambaye ameitawala nchi hii kubwa , iliyokumbwa na mizozo kwa karibu miaka 18.
Miongoni mwa wale walioko katika nafasi za mbele ni pamoja na mrithi aliyeteuliwa na Rais Kabila Emmanuel Ramazani Shadary na wagombea wawili wa upinzani, mwanasiasa wa siku nyingi mwenye ushawishi mkubwa Felix Tshisekedi na Martin Fayulu ambaye amejitokeza hivi karibuni.
Anayetafutwa ni mwanasiasa kiongozi katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini ambayo haijawahi kuwa na kipindi cha madadiliko ya amani ya utawala tangu ipate uhuru kutoka Ubelgiji mwaka 1960.
Kabila alikuwa aondoke madarakani miaka miwili iliyopita, lakini aling’ang’ania madarakani na kuzusha maandamano ya umma ambayo yalikandamizwa kikatili, na kusababisha vifo vya watu kadhaa.
Uchaguzi ambao ulitanguliwa na kucheleweshwa mara kwa mara, ulifanyika katika hali ya utulivu, lakini hali ya wasi wasi imejijenga katika muda wa kipindi cha mchakato wa kuhesabu kura.