FERDNANDA MBAMILA Na SHA BANDAR ES SALAAM
NAIBU Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Tanzania (TUCTA), Dk. Yahaya Msigwa amesema kauli ya Rais Dk. John Magufuli kutengua kanuni ya mafao ya wastaafu (kikokotoo kipya) imeleta manufaa kwa wafanyakazi baada ya kuongezewa muda.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kuhusiana na sheria hiyo, Dk Yahaya alisema alimshukuru Rais kwa kuiweka kanuni hiyo wazi kwa wafanyakazi ambayo itapitiwa upya mwaka 2023.
“Rais ameweka kanuni hiyo ili kuwapisha wadau mbalimbali nchini waje na sheria yenye tija na inayolinda maslahi ya wafanyakazi kupitia mifuko ya jamii.
Dk Msigwa aliongeza kuwa awali mifuko hiyo ilikuwa mitano lakini hivi sasa miwili baada ya kubadilishwa kwa sheria hiyo hivyo kwa namna moja imewarahisishia wadau kuondoa mkanganyiko ambao uliwaweka gizani,”alisema Dk. Msigwa.
Aliitaja mifuko hiyo ya jamii kuwa ni NSSF ambayo inahusika na sekta binafsi pamoja na PSSSF ambao niwa watumishi wa serikali.
Wakati huo huo Umoja wa Wazazi Tanzania (CCM), umempongeza Rais Magufuli kutokana na busara ya kurudisha imani kwa wastaafu ambao walikuwa wameipoteza baada ya uamuzi wa serikali kubadili kanuni ya kikokotoo kilichotumiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi, Dk.Edmund Mndolwa alisema mfumo uliokuwa umepitishwa na serikali wa asilimia 25 ulileta shida kwa wastaafu.
“Jambo hili lilileta sintofahamu ya stahili za wastaafu hao ambapo kulizuka mjadala mkubwa nchini, Umoja wa Wazazi tunampongeza kwa kuahirisha mchakato huo mpaka 2023 ili wadau wa mifuko hiyo waweze kujadiliana kwa kina kwa faida ya pande zote mbili yaani mifuko ya jamii na wastaafu,”
“Kuendelea kuwa Tanzania ya maadili mema ,utawala bora nchini na naamini nchi itasonga mbele kukiwa na mshikamano,” alisema Dk.Mndolwa.