Nape atumia muda wa kampeni kutukana
Jonas Mushi na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MJUMBE wa Kamati ya Ushindi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye ametumia muda wote aliopewa kumnadi mgombeaa urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli kumtukana mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha Ukawa, Edward Lowassa pamoja na viongozi wenzake.
Katika mkutano huo uliofanyika jana katika viwanja vya Samora mjini Iringa na kurushwa moja kwa moja katika Kituo cha Star TV, Nape alitumia muda wake wote kumtukana Lowassa pamoja na viongozi wa Chadema bila kutoa ahadi ya jambo lolote kwa wananchi.
Ingawa hakumtaja jina ni kiongozi gani wa Ukawa alikuwa akimlenga, Nape aliwataka Watanzania kuacha kumchagua marehemu kuingia Ikulu na kumuacha aliye mzima.
“Twendeni kwa wingi Oktoba 25, mwaka huu ili kuyazuia mafuriko kwa kidole.
“Nafasi ya urais ni kubwa, hatuwezi kumuweka mtu hivi hivi, hatuwezi kuchagua marehemu tukamuacha mzima nchi itakuwa ya ajabu, hatuwezi kumuacha mwadilifu na kumchagua mwizi,” alisema.
Aliongeza “Mtu mwenye historia kama hii ya Lowassa tunawezaje kumsimamisha katika nafasi ya urais… aende Ikulu inawezekanaje ni mwizi anatumia vibaya madaraka.”
“Namshangaa Mbowe, na Peter Msigwa (mbunge anayemaliza muda wake Iringa Mjini). Walisema atakayemuunga mkono Lowassa aende akapime akili yake, sasa nawaambia watangulie kupima akili maana wapo naye,” alisema.
Nape alisema Lowassa amekinunua chama hicho na kisha kuwahonga viongozi wa juu na wale waliokuwa wakimponda kama Msigwa.
“Amewaweka mezani na akawanunua wote akawatia mkononi, Mtei akapewa Sh bilioni mbili, Mbowe bilioni tatu na Msigwa akapewa milioni 340 ili kuwafumba midomo na kweli wamenyamaza kimya hadi leo,” alisema.