24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

NEC yajikanganya

6*Mkurugenzi Tehama aondolewa

* Maofisa watoa kauli tofauti

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Sisti Cariah ameondolewa kwenye nafasi hiyo, imefahamika.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya NEC ambazo MTANZANIA ilizipata juzi na jana  zimeeleza kuwa mkurugenzi huyo ambaye ni mtu muhimu katika Tume ameondolewa katika siku za karibuni huku kukiwa hakuna taarifa ya wapi alikohamishiwa   serikalini.

Chanzo hicho cha ndani ya tume kimesema  mkurugenzi huyo ameondolewa siku tano zilizopita huku zikiwa zimesalia siku 25 tu kufikia Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 wakati  idara hiyo ya Tehama ikiwa ndiyo ina orodha nzima ya Watanzania wanaotarajiwa kupiga kura.

“Ni kweli mkurugenzi huyo wa Tehama ameondolewa na nafasi yake  imechukuliwa na aliyekuwa msaidizi wake (bila kumtaja) na nafasi nyingine zinaendelea kusukwa upya.

Hadi jana   tovuti ya Tume hiyo hadi ilikuwa ikionyesha kuwapo  mkurugenzi mmoja tu ambaye ni  Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima, huku ukiwapo unaosomeka kwamba kurugenzi nyingine zinaendelea kusukwa upya.

Tume hiyo ina kurugenzi saba ambazo ni Elimu ya mpiga kura na habari, Uchaguzi, Ununuzi, Uhasibu, Ukaguzi,   Utawala na Tehama.

MTANZANIA lilipomtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari wa NEC, Clarence Nanyaro   kupata ufafanuzi wa suala hilo alisema:

“Ndugu yangu hakuna mkuu yeyote wa idara aliyehamishwa hadi sasa lakini ngoja nifuatilie zaidi nitakupa jibu zuri kwa kutumia simu ya mezani.”

Baada ya dakika chache  alipiga simu lakini  aliendelea kusisitiza kwamba anaamini idara hizo hazijafanyiwa marekebisho.

Hata hivyo alisema  hazisimamiwi na wakurugenzi   bali zinasimamiwa na wakuu wa idara.

“Watu wengi wamekuwa wakiwaita wakuu wa idara hizo kama wakurugenzi jambo ambalo si sahihi na hata hivyo wote bado wapo,” alisema Nanyaro na kuongeza:

“Sina taarifa za kuhamishwa   Dk. Cariah kwa kuwa hadi jana (juzi) alikuwa kazini akiwajibika hadi saa nne usiku tulipoachana.

Alipoulizwa kuhusu tovuti ya NEC kuwa na ujumbe unaoonyesha kufanyika  marekebisho ya wakuu wa kurugenzi zote saba, alisema suala hilo aulizwe Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumzia  wafanyakazi wa Tume.

MTANZANIA lilipomtaka asaidie kupata jibu hilo kutoka kwa bosi wake huyo alisema kwamba wakati huo mkurugenzi huo alikuwa   kwenye mkutano na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU).  Aliahidi kutoa jibu baadaye kama angeonana na Kailima na kukata simu.

Baadaye  Nanyaro alipiga tena simu na  kusema kwamba taarifa zilizokuwa zikielezea mabadiliko ya  viongozi wa kurugenzi za Tume zilitokana na viongozi hao   saba kutowasilisha picha zao kwa ajili ya kuziingiza taarifa hizo kwenye tovuti.

“Napenda kusema wakurugenzi wote saba wapo kazini; katika Idara ya elimu ya mpiga kura na habari, Uchaguzi, Ununuzi, Uhasibu, Ukaguzi na Utawala akiwamo Dk. Cariah wa Tehama ambaye alikuwa kazini hadi juzi na alitoka muda wa saa nne usiku,” alisema Nanyaro.

Kauli ya Jaji Lubuva

Wakati Nanyaro akisema hivyo, juzi  Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alipoulizwa na Mtanzania  alikiri kuwa Mkurugenzi huyo wa Tehama, Dk. Cariah,  amehamishwa.

Hata hivyo  dakika chache baadaye Jaji Lubuva alipiga simu kwa mhariri wa gazeti hili akikanusha taarifa yake hiyo ya awali akisema  hakuna mkurugenzi yeyote aliyehamishwa katika Tume yake tofauti na mabadiliko yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika nafasi ya mkurugenzi wa uchaguzi iliyokuwa inashikiliwa na Julius Malaba ambaye aliteuliwa kuwa jaji hivi karibuni.

“Nakwambia ndugu yangu, Mbowe na Chadema waache kutapatapa, wanaingilia utendaji wa Tume na serikali nawaomba wasiendelee kupotosha umma, ” alisema Jaji Lubuva.

Alichosema Mbowe  

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Himo Polisi mkoani Kilimanjaro juzi, Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe aliituhumu Serikali kwa kile alichokiita uchakachuaji wa NEC kwa kubadilisha wakurugenzi wote na kuweka wapya kutoka idara nyeti za usalama.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alidai  viongozi hao wa Tume wameondolewa na serikali  lengo likiwa ni kuiba kura.

“Mtu mwenye wajibu wa sheria wa kusimamia uchaguzi ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi,  baada ya CCM kuona Lowassa (Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa),  anashinda wameamua kuandaa mazingira ya kuchakachua Tume yenyewe.

“Walianza kumuondoa Mkurugenzi wa Tume Malaba (Julius)  mwezi mmoja uliopita katika  mazingira ya kutatanisha wakaleta mwingine, wiki mbili zilizopita…. wakurugenzi wote wamewang’oa na kuwaingiza wengine.

“Tume kwa sasa siyo huru huku Serikali ya CCM pia ikiingiza wanajeshi kwenye tume hiyo.  Namuuliza Mkuu wa Majeshi atueleze  hao wanajeshi huko wameenda kufanya nini?” aliuliza Mbowe

Mbowe alisema pia kuwa CCM imeanza mkakati mwingine wa kutengeneza kura bandia na tayari  zimepelekwa mkoani Kilimanjaro, Mamlaka ya Barabara (Tanroads) ambayo iko chini ya Magufuli ndiyo inasambaza kura hizo,” alidai  Mbowe.

Mwenyekiti mwenza huyo wa Ukawa alisema hakuna mkakati wowote ovu utakaopangwa na CCM bila Umoja huo kuujua kwa sababu kila inachokipanga asubuhi wao wanakipata mchana.

“Mnaopanga nao mchana, usiku tunakuwa nao. Kikwete wewe ni rais wa nchi  usifikiri una usalama sana kama utaharibu uchaguzi wa nchi hii. Watanzania ndiyo wataamua, Kikwete na familia yako hamtatuchagulia mtu, tumia majeshi, tumia vyote unavyotaka, tutapiga kura na kuzilinda kwa gharama yoyote… nimesema haya nitoe onyo kwa CCM,” alisema Mbowe.

Akiwa kwenye mkutano wa kampeni   katika Kata ya Kahe kwenye Viwanja vya Shule ya Oria, Mbowe alisema kila mtu atakayejaribu kuzuia mabadiliko na kuwa wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ya masilahi binafsi, mafuriko yatamkumba.

“Mabadiliko tunayozungumzia hapa yako kwa vyama vyote, mtu yeyote atakayekuwa wakala wa kuitetea CCM kwa sababu ya ubinafsi mafuriko lazima yamkumbe, tuna kila sababu ya kupigania mabadiliko,” alisema Mbowe.

Alisema mabadiliko ambayo Ukawa unayapigania  yanamgusa kila Mtanzania bila kujali dini yake wala kabila lake hivyo ni vigumu mtu   kuyahujumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles