Leah Mushi, Dar es Salaam
Imekuwa kawaida kwa jamii ya kitanzania kushiriki na watoto wanaolelewa katika vituo vya watoto wenye uhitaji chakula na mahitaji mengine hususan katika msimu wa sikukuu
Mwananchi mmoja mmoja, vikundi taasisi na ofisi mbalimbali za serikali na binafsi zimekuwa zikitoa msaada wa chakula na mahitaji mengine kwa vituo vya watu wenye uhitaji lakini je umeshawahi kujiuliza watoto hao wanahitaji nini zaidi?
“Mimi napenda sana mtu anipeleke kuogelea, sisi tunataka kutoka na kujumuika na watoto wengine tucheze nao na tufurahi badala ya wao kuja kutuachia chakula tu na kuondoka,” anasema Mudy Mbeki mtoto anayelelewa katika kituo cha Yatima Group Trust Fund kilichopo Chamazi.
Mudy ni mmoja kati ya watoto zaidi ya 250 kutoka vituo viwili vya watoto wenye uhitaji vya Yatima Group Trust Fund Chamazi na Kurasini Orphanage Center waliokutanishwa pamoja katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kusherehekea na wafanyakazi pamoja na wadau wa Serena msimu huu wa sikukuu.
“Tumekodi zaidi ya magari matano kwenda kuwafuata watoto katika vituo vyao Kurasini na Chamazi ili waje hapa Serena Hotel tufurahi nao sikukuu hii, na huu ni utamaduni wetu wa miaka mingi baada ya kugundua watoto wanataka sana kutoka nje ya makazi yao waliyozoea kipindi hiki cha sikukuu” amesema Meneja Rasilimali Watu wa Hoteli ya Serena, Sophia Mketo.
Amesema katika kuandaa sherehe hiyo, wameshirikiana na wadau wa Serena kwa kuwanunulia zawadi watoto wote waliofika hapo kwenye sherehe na lengo kuu ni kuhakikisha watoto wanakuwa na furaha na kuona wanathaminiwa.
“Awali tulikuwa tukipika chakula na kupeleka vituoni lakini watoto hao ndiyo walioonesha hamu ya kutaka kutoka nje ya vituo ndipo tulipoanza utamaduni wa kuwatoa ‘outing’ na imeendelea hivyo kwa miaka mitatu mfululizo sasa,” amesema.
Pamoja na kuwaandalia chakula cha mchana, zawadi na michezo mbalimbali Hoteli ya Serena pia ilimualika mchekeshaji maarufu, Stan Bakora ambaye naye aliwaelezea watoto hao historia ya maisha yake kuwa akiwa mdogo pamoja na wadogo zake wawili walifiwa na wazazi wao na walilelewa na bibi yake ambaye baada ya miaka kadhaa naye alifariki na hivyo yeye kuchukua jukumu la kuwalea wadogo zake kwa kutumia kipato alichopata kupitia sanaa yake ya uchekeshaji.
Mbali na kuwachekesha na kuimba na watoto hao waliokuwa na sura za furaha aliwakaribisha wanajamii wote kuwasiliana naye iwapo watataka ajumuike na watoto yenye uhitaji siku yoyote.
“Mimi ni yatima kama ninyi, lakini nina ndoto kubwa na namshukuru Mungu kidogo naweza kujimudu na kusomesha wadogo zangu hivyo msikate tamaa na iwapo kuna yeyote atataka kunitumia kushiriki na watoto kama leo walivyofanya Serena nawakaribisha tuwasiliane,” amesema.
Naye Katibu Mtendaji wa Kituo cha Yatima Group Trust Fund Chamazi, Fred Njegeja, ameshukuru wanajamii kwa mchango wanaoutoa katika kituo hicho na kuwaomba kuzingatia hitaji la watoto kutoka nje ya kituo na kujichanganya na wanajamii katika kusherehekea sikukuu.
“Hapa kituoni kwetu asilimia 95 ya msaada unatoka kwa wanajamiii na wanakuja si tu kipindi cha sikukuu lakini na wakati mwingine tu wakiwiwa kutoa msaada kwa watoto katika kituo chetu, lakini kipindi hiki cha likizo ni vyema hata mwenye uwezo wa kuchukua watoto watani akatoka nao ‘outing’ inawasaidia sana wanakuwa wanafurahi na kuona wanathaminiwa,” amesema.
Amesema hali ya kutoka nao nje ya maeneo ya kituo ni kitendo kizuri kwakuwa watoto wengi katika kituo hicho ni wale ambao wamefukuzwa makwao au wazazi wao wamefariki hivyo wamejijenga katika fikra ya kuwa hawapendwi, hivyo kuwachukua kucheza nao na kushiriki nao chakula nje ya makazi yao kunaongeza sana morali na kuona kuwa wanathaminiwa.