Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Isack Aman, amewataka Watanzania kuendelea kuliombea taifa ili liwe na amani inayosimamiwa kwa sheria.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa katika ibada maalumu iliyoandaliwa na Umoja wa Makanisa Mkoa wa Arusha na kuhubiriwa na Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo.
Akizungumza wakati wa kutoa salamu ikiwa mara yake ya kwanza kushiriki ibada hiyo tangu aliposimikwa kuongoza jimbo hilo, Askofu Aman alisema Tanzania ni nchi ya Watanzania wote na amani inayoombwa imekuwa tunu ya wote.
“Tunamshukuru Mungu kwa utulivu huu, nchi nyingine si kama ilivyo hapa kwetu, hivyo tunapotafakari kuhusu amani ni lazima tuwe na mahali pa kusimamia.
“Kwanza haki lazima isimamie amani, hii nchi ni yetu wote. Tupo hapa leo (jana) kushirikiana kuombea amani taifa letu na viongozi ni muhimu tuwe na amani inayosimamiwa na sheria,” alisema Askofu Aman.
Katika salamu hizo, Askofu Aman alitumia fursa hiyo kuzipongeza juhudi na mipango mbalimbali inayofanywa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo na kuwaomba wabunge, viongozi wa Serikali na wananchi kuendelea kushirikiana.
“Ushirikiano huu unaendelea kutufanya Watanzania kufurahia uhuru utokanao na kutenda kazi,” alisema Askofu Aman.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), Dk. Stanley Hotay alipongeza kupungua kwa kasi ya vitendo vya rushwa huku akitahadharisha kuhusu hatari mpya ya kamari ya kisasa kwa vijana.
Kutokana na hatari hiyo kwa vijana, Askofu Dk. Hotay aliiomba Serikali kuangalia kwa makini suala hilo kwani limeendelea kuchochea uvivu miongoni mwa vijana.
“Hizi kamari tunaziona kila kona ya miji mikubwa, zinachochea uvivu miongoni mwa Watanzania, lakini pia sehemu kubwa ya fedha hizo huenda nje ya nchi, ni vyema Serikali ikaliangalia jambo hili.
“Kamari zinazochezeshwa kwa kuchangisha vijana shilingi 1,000 na kisha kuwapa mamilioni ya fedha zinachangia uvivu wa kufanya kazi ngumu zinazoleta maendeleo.
“Vitendo hivi vitazidi kuzalisha masikini nchini, utajiri hauwezi kuletwa au kuja kwa kukaa kwenye televisheni na kuvuna mamilioni ya fedha kwani kuzaliwa kwa Yesu Kristo kumeleta mawazo mapya ya kujikomboa.
“Afrika ni bara tajiri, lakini watu wake masikini, tuna rasilimali nyingi sana asilimia 30-37, lakini tunachangia asilimia 3 tu ya uchumi wa dunia,” alisema Askofu Dk. Hotay.
Akisisitiza kuhusu amani na utulivu katika mahubiri yake, aliviomba vyombo vya ulinzi kuwafundisha ikiwamo vyenyewe kutenda haki kwa watu.
“Vyombo vya ulinzi tendeni haki, wale wakarofi waadhibiwe na si kuadhibu wote hata wasio wakorofi, kuna namna mbili ya kumpeleka punda, kwanza kumpiga fimbo lakini kumpa majani. Punda anayepewa majani siku zote hufikisha mzigo,” alisema Askofu Dk. Hotay.
Naye Mkuu wa Mkoa Gambo, aliwashukuru viongozi wa dini kwa kuchangia kwa kiwango kikubwa suala zima la amani kutokana na kukutana na wananchi kila wakati.
“Viongozi wa dini kila mkikutana na wananchi hawa mnasisitiza amani, kwa mtazamo wangu amani ya Arusha imechangiwa kwa asilimia 90 na viongozi wa dini huku asilimia 10 ikiwa ni Serikali,” alisema Gambo.
Aidha akisisitiza suala zima la amani wakati wa Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’anzi, alisema wameimarisha ulinzi kila kona ya mkoa huo.
“Tumejipanga kufanya doria za kutosha zitakazokuwa na mbwa na askari polisi kila kona kuanzia maeneo ya nyumba za ibada,” alisema RPC Ng’anzi.