PATRICIA KIMELEMETA
WANAFUNZI wawili wa darasa la pili wa shule za msingi Mtoni Kijichi na Bwawani, zilizopo Manispaa ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam, Nasir Mustafa(mtoni kijichi) na Swabra Salum(Bwawani) wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa uzio wa shule hizo huku wengine watatu wakijeruhiwa vibaya.
Mashuhuda wa tukio hilo walipozungumza na gazeti hili jana walisema tukio hilo lilitokea majira ya 2.45 asubuhi wakati wanafunzi hao walipofika shuleni kwa ajili ya kuchukua ripoti za matokeo ya mitihani ya kufunga shule.
Walipofika kwenye eneo la ukuta huo wakiwa wanacheza, mara ukuta huo ulianguka na kuwafunika wanafunzi hao hali iliyosababisha vifo na wengine kujeruhiwa.
“Ndani ya shule kuna korongo kubwa ambalo kila siku linaongezeka kutokana na mchanga uliopo pale, ukuta upo karibu na korongo hilo, hivyo basi wanafunzi wapofika kwenye eneo hilo huku wakiwa wanacheza, wakaangukiwa na ukuta na kusababisha kifo na majeruhi,” alisema Said Juma shuhuda wa tukio hilo.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtoni Kijichi, Evelyne Munishi, alisema kuwa, wanafunzi hao walikua wanacheza baada ya kumaliza mitihani yao ya muhula na walifika shuleni hapo kwa ajili ya kuchukua ripoti zao ili wasubiri kufunga shule leo.
“Ni kweli ukuta umeanguka na mwanafunzi mmoja katika shule yangu wa darasa la pili (Nasir) amefariki huku mwenzake wa darasa la tatu, Sharifa Jumanne akijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupatiwa matibabu,”alisema Mwalimu Munishi.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bwawani, Mary Shayo, alisema tukio hilo limesababisha kifo cha mwanafunzi mmoja wa darasa la pili katika shule yake na majeruhi wawili.
“Wanafunzi walikua wanacheza huku wakisubiri ripoti zao, bahati mbaya ukuta ukaanguka na kusababisha kifo cha mwanafunzi Swabra huku wawili wakijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Temeke kwa ajili ya matibabu,” alisema.
Aliwataja majeruhi hao ni Mukrimu Stambul na Rehema Idd wote wa darasa la pili ambao kwa sasa wanaendelea na matibabu Hospitali ya Temeke.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Butiama zilipo shule hizo, Hajji Mgaya, alisema tukio hilo ni la kusikitisha kwa sababu limeleta vifo kwenye mtaa wao.
“Tumesikitishwa sana baada ya kusikia ukuta umeanguka na kuua wanafunzi wawili, tunawaombea kwa Mungu majeruhi wapone haraka,”alisema Mgaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emanuel Likula, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tayari Jeshi la Polisi limefuata taratibu za kisheria ili wanafunzi waliofariki waweze kuzikwa na waliojeruhiwa waweze kupata matibabu.
“Ni kweli wanafunzi wawili wamekufa na watatu wamejeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa uzio wa shule mbili za Mtoni Kijichi na Bwawani, tayari tumemaliza taratibu za kisheria zimefuatwa hivyo basi wazazi wanaweza kuchukua miili na kuzika,”alisema Kamanda Likula.