27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ateta na kachero nguli

*Ni aliyekuwa Mkurugenzi wa usalama enzi za Mkapa na Kikwete

Na Mwandishi Wetu

RAIS Dk. John Magufuli, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Apson Mwang’onda, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, Apson amesifia utendaji kazi wa Rais Magufuli.

Taarifa hiyo ilisema baada ya mazungumzo ya wawili hao, Apson alimshukuru Rais Magufuli kwa kukubali ombi lake la kumwona na kuzungumza nae.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Apson alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi mzuri unaochochea kasi ya maendeleo hususani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendelo.

Apson ambaye ni kachero nguli hapa nchini, aliitaja baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Rais Magufuli kuwa ni mradi wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers’ Gorge Power Project) na ujenzi wa madaraja na barabara ambazo licha ya kurahisisha usafiri, zitasaidia kuondoa msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

“Mabadiliko ni makubwa sana ambayo yametokea, kuna miradi mikubwa mingi inafanyika sasa hivi, kwa hiyo mabadiliko ni makubwa kusema kweli na yote hayo ni kwa manufaa ya nchi, kwa hiyo nachoweza kusema amefanya kazi kubwa kwa maendeleo ya nchi” taarifa ya Ikulu ilimnukuu Apson.

Ilisema Apson alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya awamu ya tano ili itekeleza mipango yake kwa ufanisi na kwa manufaa ya Taifa.

Apson ambaye alihudumu kwenye idara hiyo kwa muda mrefu, alikuwa Mkurugenzi wa idara hiyo kwa kipindi cha miaka 10 ya Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Baada Mkapa kumaliza muda wake, Apson aliendelea kuhudumu katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete, hadi Rashid Othman alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Othman, aliteuliwa kushika wadhifa huo na Kikwete, Agosti 20, 2006,  akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Apson aliyestaafu Agosti 21, mwaka 2006 kwa mujibu wa sheria.

Waliowahi kuongoza usalama

Kwa miaka kadhaa idara hiyo iliongozwa na vigogo kadhaa waliobobea katika masuala la Ulinzi na Usalama wakiwamo, Emir Mzena, Lawrance Gama, Hans Kitine ambapo alipoondoka nafasi hiyo ilikamatwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga.

Mbali na hao nafasi hiyo ilishikiliwa pia na Amrani Kombe na baadae Apson na Othman kabla ya Rais Magufuli Agosti 24 mwaka 2016 kumteuwa Dk. Modestus Kipilimba, kushika nafasi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles