29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Afrika yachangia kuongezeka kwa surua duniani

SURUA ni moja ya magonjwa ya kuambukiza yanayotishia maisha ya mwanadamu.

Ni ugonjwa ulio na kiwango cha juu cha karibu asilimia 100 cha mashambulizi pindi mtu apatapo vimelea vya ugonjwa huu.

Pamoja na kuwapo chanjo ya ugonjwa huu, bado surua ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vingi vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano katika baadhi ya maeneo duniani hasa kwa nchi zinazoendelea.

Ugonjwa huu ambao ulitoweka katika baadhi ya nchi, umeanza kuonekana tena hivi karibuni miongoni mwa watu ambao hawakupata chanjo katika nchi za Uingereza na nyingine za Ulaya

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN), ugonjwa huu duniani uliongezeka kwa zaidi ya asilimia 30 mwaka uliopita, ikilinganishwa na mwaka 2016, huku ongezeko likishuhudiwa zaidi katika mataifa yaliyoendelea ya Ulaya kutokana na kile kinachodaiwa wasafiri kutokea Afrika.

Shirika ya Afya Duniani (WHO), limesema hali ya wasiwasi wa kugundulika kwa wagonjwa wapya surua unakaribia kuwa tukio linaloihusu dunia kwa ujumla, lakini sababu zinatofautiana miongoni mwa maeneo.

Katika Bara la Ulaya, wataalamu wamesema tatizo hilo linatokana na habari mbaya kuhusu chanjo ya surua ambayo imethibitishwa kuwa bora na salama.

Mkuu wa masuala ya chanjo wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Martin Friede, anasema kashfa inayotolewa na baadhi ya wanaojiita wataalamu kuhusu chanjo hiyo bila kuwa na ushahidi, imeathiri uamuzi wa wazazi.

Anakosoa madai yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba chanjo hiyo inasababisha matatizo.

Lakini wagonjwa wa surua wameongezeka katika Amerika ya Kusini kutokana na kudhoofu kwa mifumo ya afya nchini Venezuela.

Ripoti hiyo ya UN inakuja huku nyingine ya WHO iliyotolewa Agosti mwaka huu, ikieleza uwapo wa ongezeko kubwa la ugonjwa wa surua barani Ulaya.

Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya watu 41,000 wameambukizwa maradhi hayo katika miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2018 barani humo.

Mwaka jana kulikuwa na kesi 23,927 barani humo na mwaka juzi kulikuwa na kesi 5,273 tu, mwenendo unaoonesha ongezeko la haraka kwa kipindi kifupi tu..

Wataalamu wa afya wanalaumu ongezeko kubwa la idadi ya watu kuwa sababu ya wimbi kubwa la maambukizo ya ugonjwa huo, huku wengi wakiacha kuzingatia chanjo.

Uingereza kumetokea kesi 807 hadi sasa kwa mwaka huu, hali iliyolifanya WHO kuyataka mataifa ya Ulaya kuchukua hatua thabiti.

Wizara ya Afya nchini Uingereza inasema mlipuko wa ugonjwa huo umetokana na idadi kubwa ya watu kusafiri katika maeneo ya Bara la Ulaya ambayo yana maambukizi.

Maambukizi yanaweza kudumu kwa muda wa siku saba na zaidi.

Lakini watu wengi waliopona kabisa hubaki na athari mbalimbali kama vile; madhara kwenye ubongo, homa kali, kupungua kwa mwili, nimonia na matatizo ya ini.

Utafiti uliofanywa miaka 20 iliyopita unaonyesha namna gani watu hawatilii maanani chanjo kama ilivyo kwenye matatizo ya mtindio wa ubongo.

Wizara ya Afya nchini humo inawataka watoto wote kupata chanjo kabla ya kutimiza umri wa mwaka mmoja na kabla hawajaanza kwenda shule.

Ukraine ina idadi kubwa ya ugonjwa wa surua barani Ulaya, ikiwa na zaidi ya watu 23,000 walioathirika. Lakini kuna nchi nyingine sita barani Ulaya ambazo zina maambukizi zaidi ya 1,000,  ambazo ni Ufaransa, Georgia, Ugiriki, Italia,Urusi na Serbia.

Vifo vingi vilivyosababishwa na surua vimeripotiwa katika nchi zote hizo Serbia ikiwa inaongoza kwa idadi kubwa ya watu 14 kufariki dunia.

WHO inasema mataifa mengi yakiwamo Ujerumani, Urusi na Venezuela wamepokonywa cheti cha kukabili surua katika muda wa mwaka mmoja uliopita. Taifa hupoteza cheti hicho wakati virusi vya ugonjwa huo vikisambaa kwa zaidi ya miezi12 mfululizo.

Hata hivyo, shirika hilo limesisitiza kuwa mapambano dhidi ya surua duniani yameonyesha matokeo mazuri katika karne hii.

Kulingana na miongozo ya WHO, kukabili surua kunahitaji asilimia 90 ya chajo katika awamu ya kwanza.

Chanjo hiyo imekuwa ikitolewa kwa asilimia 85 kwa miaka mingi, lakini kiwango hicho ni cha chini katika maeneo ya Afrika, ambayo yalikuwa na asilimia 70 mwaka 2017.

Surua ni ugonjwa unaombukizwa ambao unaweza kusababisha kuharisha vibaya, homa ya mapafu na kupoteza uwezo wa kuona na wakati mwingine kusababisha vifo.

Mwaka uliopita mambukizi 190, 000  na vifo 110, 000 vilinakiliwa kote duniani, lakini idara ya afya ya Umoja wa Mataifa inakadiria kuwa idadi kamili ni watu milioni 6.7. Wagonjwa wengi waliofariki dunia walikuwa watoto.

Dalili za maradhi ya surua ni pamoja na kuhisi baridi na kupiga chafya, homa kali, uchovu, kukosa hamu ya kula na misuli kuuma, macho kuwa na rangi nyekundu na majimaji na rangi ya kijivu mdomoni.

Kuwa na vipele vyenye rangi nyekundu ambavyo vinaweza kusambaa kutoka kwenye kichwa, shingoni na mwilini kote.

 

Surua husababishwa na nini?

Ugonjwa huu huenezwa na aina ya virusi jamii ya paramyxovirus. Virusi hivi hupatikana katika mfumo wa njia ya hewa. Hukaa katika kamasi na majimaji yaliyopo katika mfumo wa hewa. Kwa sababu hii basi virusi hawa huenezwa kwa njia ya upumuaji.

Virusi hawa wanaweza kuishi hewani kwa muda wa hadi saa moja baada ya kutolewa kwa kupiga chafya au kukohoa au hata mazungumzo na mgonjwa. Hii ina maana kuwa, ili kuambukizwa surua, si lazima mtu akutane ana kwa ana na mgonjwa.

Baada ya kuingia ndani ya mfumo wa hewa virusi hushambulia seli za utando wa nje wa njia ya hewa (respiratory tract epithelium) na kuingia katika mzunguko wa limfu na kufika kwenye tezi zilizo karibu. Katika tezi huzaliana zaidi na kusambaa mwilini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles