WASHINGTONDC,Marekani
WIZARA ya Ulinzi imesema maelezo zaidi juu ya mipango ya maziko ya Rais Mstaafu, George H. W. Bush, ambaye alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 94, yanaandaliwa na familia yake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na wizara hiyo, Rais Bush ambaye alitumikia nafasi ya urais tangu mwaka 1989-1993, ataagwa kwa heshima zote za taifa kesho katika Kanisa Kuu la Washington na kuzikwa Alhamisi katika makazi yake katika Jimbo la Texas.
Ilieleza baada ya jana maandalizi hayo kuwa tayari, mwili wake ungewekwa katika ukumbi wa Rotunda ndani ya bunge la hapa kwa ajili ya wananchi kuuaga mpaka kesho asubuhi, wakati utaratibu wa kupewa heshima zote za taifa uliondaliwa jana.
Tarifa hiyo ilieleza zaidi kwamba umma wa Wamarekani utaweza kuendelea kutoa heshima za mwisho wakati mwili wa Rais Bush ukiwa katika jeneza kuanzia jana saa 1:30 asubuhi hadi Jumatano majira kama hayo.
Ikulu ilitangaza juzi kuwa Rais Donald Trump atahudhuria shughuli za kuuaga mwili wa wa kiongozi huyo.
Msemaji wa Ikulu, Sarah Sanders alisema kesho imepangwa kuwa siku ya taifa ya maombolezi na bendera ndani ya Ikulu tayari zimeshushwa nusu mlingoti kumuenzi kiongozi huyo.
Katika hatua nyingine, mbwa ambaye alikuwa akimuhudumia kiongozi huyo amepigwa picha akiwa amelala kando ya jeneza kama sehemu ya kutoa heshima zake za mwisho.
Mbwa huyo anayeitwa Sully, jana alitarajiwa kusafiri kwa ndege pamoja na jeneza lenye mwili huo kutoka mjini Texas hadi hapa ambako ulitarajiwa kuanza kuagwa.
Picha iliyotumwa kwa njia ya mtandao wa Twitter na msemaji wa Rais Bush, Jim McGrath,inamuonyesha mbwa Sully akiwa kando ya jeneza ikiwa na ujumbe unaosema ‘Mipango imekamilika’.