25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Matukio 20 yaacha alama 2018

Na AGATHA CHARLES


IKIWA hii  ni wiki ya kwanza ya mwezi Disemba, ambao ni wa mwisho kwa mwaka huu,  matukio 20 yameonekana kuacha alama au kumbukumbu nchini.

KUTEKWA MO

Tukio ambalo tunaweza kusema pasipo shaka ndilo lililotikisa zaidi si tu hapa nchini bali pia nje ya nchi kutokana na namna lilivyoleta mshtuko na hata lilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa, ni lile la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji (Mo).

Tukio la kutekwa kwa Mo ambaye anatajwa na jarida maarufu duniani la Forbers kama bilionea kijana barani Afrika lilitokea alfajili ya Oktoba 11, mwaka huu wakati mfanyabiashara huyo alipokuwa akiingia mazoezini katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Baada ya kupita takribani siku tisa za Jeshi la Polisi kumsaka hatimaye Mo alipatikana akiwa ametelekezwa na watekaji hao kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Kipolisi Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Lazaro Mambosasa ndiye alithibitisha kupatika kwa Mo alifajiri ya Oktoba 20, mwaka huu.

Alisema Mo aliwaeleza kuwa watekaji hao walimpeleka eneo ambalo walitumia takribani dakika 15 kabla hawajamweka katika chumba kilichokuwa na godoro alilotumia kulala.

Kamanda Mambosasa alisema watekaji hao walizungumza lugha ambayo Mo aliitambua kuwa ni moja ya zilizoko nchini Afrika Kusini.

Novemba 11, mwaka huu, Kamanda Mambosasa aliwaonyesha wanahabari nyumba ya ghorofa moja iliyopo Mbezi Beach, Dar es salaam iliyodaiwa kuhifadhiwa mfanyabiashara huyo.

Alieleza kuwa watekaji hao walipanga hapo kabla ya kufanya tukio hilo huku wakijitambulisha kuwa ni wafanyabiashara wa madini kutoka Afrika Kusini.

Alisema watekaji wa Mo walipanga nyumba hiyo kupitia kwa dereva wa taxi anayejulikana kama Twalib Mussa mwenyeji wa Tanga ambaye Jeshi la Polisi  lilimshikilia.

SAKATA LA KOROSHO

Mjadala wa zao la korosho ambao umesababisha hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli aingilie kati kwa kuliangiza Jeshi la Wananchi (JWTZ) kuzinunua na kuhifadhi,  uliibuka tangu mwaka jana baada ya bei kupanda hadi Sh. 4,000 kwa kilo.

Juni, mwaka huu, mjadala kuhusu zao hilo na bei  yake ulitinga bungeni wakati serikali ilipowasilisha muswada wa mabadiliko ya sheria kuhusu mgawanyo wa fedha za ushuru kabla ya bei kushuka msimu huu.

Mzozo wa korosho ulikolea zaidi baada ya wakulima kugomea bei mpya kati ya Sh1,900 hadi Sh2,700 kwa kilo ikiwa ni anguko la kutoka wastani wa Sh 4,000 kwa kilo msimu uliopita.

Wakulima wa zao hilo katika mikoa ya Lindi na Mtwara waligoma kuuza zao hilo kwa kile walichokidai kushuka kwa bei ukilinganisha na miaka miwili iliyopita huku gharama za uzalishaji zikiwa zimepanda.

Kutokana na mgomo wa minada ya siku mbili, Oktoba 26, Rais Magufuli, alimuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwaeleza kuwa anaunga mkono hatua ya uamuzi huo kwamba yuko nao bega kwa bega.

Oktoba 28, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya kikao na wanunuzi wakuu wa zao hilo na kuwaeleza kuwa serikali inaunga mkono msimamo wa wakulima na kwamba hayuko tayari kuona korosho hizo zikiuzwa chini ya Sh. 3,000 kwa kilo.

Rais Magufuli alienda mbali kwa kusema serikali  ipo radhi kuzinunua korosho zote kwa bei inayowafaa wakulima na kuziuza katika masoko ya kimataifa nchini Marekani na China.

Novemba 10, sakata hilo la korosho lilichukua sura mpya baada ya Rais Magufuli kuwaondoa mawaziri wawili katika baraza lake akiwamo aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.

Magufuli aliliagiza JWTZ kwenda kufanya kazi hiyo ya kununua korosho hizo kwa gharama ya shilingi 3,300 na alikagua magari 75 yenye uwezo wa kubeba tani 1,500.

RUSHWA YA NGONO

Habari nyingine ambayo imeonekana kugusa wengi na hata kuibua mjadala wakati tukielekea ukingoni mwa mwaka 2018 ni ile iliyoibuliwa wiki hii na Mhadhiri Mwandamizi  wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk. Vicensia Shule akidai rushwa ya ngono imetawala chuoni hapo.

Dk. Shule aliibua tuhuma hizo kupitia katika akaunti yake ya Twitter, ambako aliandika;  “Baba MagufuliJP (Rais John Magufuli) umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM.

“Nilitamani nikupokee kwa bango langu ila ulinzi wako umenifanya ninyamaze. Nasubiri kusikia toka kwako maana naamini wateule wako ni waadilifu watakwambia ukweli”.

Suala hilo limenekana kuwasha moto baada ya Kamati ya Maadili ya chuo hicho (CKD), kumwita na kukutana na Dk. Shule juzi na kuwaeleza kuwa suala hilo tayari amelifikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Hatua hiyo ni kama imechochea moto kwa vyuo vingine wani juzi Takukuru mkoani Mwanza ilikiri kumuhoji Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) (jina tunalihifadhi kwa sababu za maadili) kwa tuhuma za kuhusika na rushwa ya ngono kwa wanafunzi wake.

KUFUTWA FIESTA

Usiku wa Novemba 23, kulisambaa taarifa ya kusitishwa kwa tamasha la kila mwaka la burudani maarufu kama Fiesta ambalo linaonekana kuwa kiungo cha mafanikio ya wasanii wengi nchini.

Tamasha hilo ambalo lilikuwa lifanyike katika uwanja wa Leaders jijini Dar es Salaam kusitishwa kwake kulitokana na maelezo yaliyotolewa na Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Kinondoni, F. Kombe kwamba walipokea malalamiko  ya makelele kutoka kwa wananchi na wagonjwa waliolazwa hospitalini.

Kusitishwa kwa tamasha hilo kulizua mjadala hadi juzi Mkurugenzi wa Kinondoni, Aron Kagurumjuli alipotoa taarifa ya kupiga marufuku shughuli yeyote kufanyika katika uwanja huo.

ITAENDELEA WIKI IJAYO

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles