26.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 6, 2021

Membe kuhojiwa urais 2020

HARRIETH MANDARI na AGATHA CHARLES, DAR/GEITA


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amemtaka aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, kufika ofisini kwake ili kutoa ufafanuzi wa tuhuma za kuandaa mpango wa kumkwamisha Rais Dk. John Magufuli kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Tayari Membe ameitikia wito wa Bashiru kupitia andiko lililosambazwa juzi usiku katika mitandao ya kijamii lakini akitoa masharti ya kukutana naye.

Hata hivyo, masharti hayo ikiwamo la kuwapo Musiba katika kikao hicho ambaye Membe anadai ndiye anayemzushia tuhuma hizo, yalikataliwa na Bashiru.

Akizungumza tena mkoani hapa jana, Bashiru, alisema CCM kilishinda maeneo mbalimbali ikiwamo Liwale (Lindi) na majimbo mengine ya Babati, Simanjiro, Serengeti, Ukerewe, Siha na Kinondoni kutokana na mshikamano wa chama hicho lakini hakuwahi kumuona Membe.

“Kote huko tumeshinda kwa sababu ya mshikamano wa wanachama. Nikasema Membe sikuwahi kupata simu yake, wala mchango wake, wala mawazo yake hata nilipoenda Lindi anakotoka ambako amewahi kuwa mbunge wake, nimekaa pale siku tatu naomba kura, sikumuona nikasema yuko wapi, mbona nasikia wanamzungumza hivi na vile, aje ana haki ya kuniona, aje tujenge chama baada ya hapo imekuwa habari ya mjini,” alisema.

Bashiru alisema amemtaja Membe kama mwana CCM kwa sababu hana nguvu kuliko chama hicho hivyo anahitaji kukutana na mwanachama huyo ofisini kwake bila kuwa na masharti yoyote.

“Ile Twitter inaweka masharti ya kukutana na mimi, wakati nimesema kwa nia njema baada ya kusoma haki na wajibu wa mwanachama, na mimi katika vitabu vyangu sijaona kama Membe amepoteza uanachama, na kama ameacha uanachama sijasikia popote anatangaza. Namtambua kama mwanachama. Ile Twittr inaeleza kwamba amenisikia lakini inaweka masharti ya kukutana na mimi. Hapana. Tunakutana na wanachama kama wanachama bila masharti na kwa taratibu na bado namhitaji,” alisema.

Bashiru alisema angekuwa na namba ya simu ya Membe angekuwa tayari ameshampigia kwa sababu anamhitaji kwa kuwa ni mtu muhimu katika umoja huo.

“Tuna rekodi mbaya katika chama, mgombea urais akinuna tunapata tabu sana, na hatutaki kuendeleza mnuno wa wale wanaotafuta vyeo wakivikosa wanatuvuruga. Nalisema kwa vyeo vyote wagombea urais, ubunge, udiwani, hatutaki makundi tena katika chama chetu, tumeumizwa vya kutosha na makundi, uongo, fitina, ubinafsi, ubaguzi na matumizi mabaya ya fedha katika siasa, tulifikia mahala wagombea wa CCM wanaomba kura makanisani,” alisema.

Pia alisema Membe hana tofauti na wanachama walioingia siku hiyo ndani ya chama kwa sababu tofauti yake ni kwamba amewahi kuwa waziri, mbunge na kiongozi wa CCM.

“Kwa nafasi yake na uzoefu wake na yanayosemwa mtaani ningehitaji kukutana naye tukazungumza. Imekuwa habari kubwa. Mimi sikusema kama mtu maalumu au maarufu, nilisema kama mfano tu inategemea wakati huo umeangukia nani, jana ulimwangukia Membe. Sio kwa sababu ni mtu maarufu au ana nguvu, au mtu muhimu hatuwezi kuendelea kujenga chama lakini ni mtu muhimu kwa sababu ni mwanachama, nguvu ya CCM inatokana na umoja wetu,” alisema.

 ONYO KWA WANACHAMA

Juzi akiwa mkoani Geita katika kikao cha viongozi wa CCM wa mkoa huo, Bashiru, alitoa onyo kali kwa wanachama waliopo na wasio madarakani akiwamo Membe kuacha tamaa ya kuwania uongozi badala yake wakijenge chama hicho.

“Iweje watu waseme (Membe) unafanya vikao vya kutafuta kura za mwaka 2020, kwamba unataka kumkomesha Rais Magufuli halafu unakaa kimya tu, sasa nakualika uje ofisini kama ni mwanachama wa kweli aliyetoa ahadi ya uanachama wa CCM ya kusema kweli daima fitina kwangu mwiko, njoo ofisini,” alisema.

Pia alisema kati ya wanachama wote wa CCM waliotia nia ya kugombea urais mwaka 2015, Membe peke yake hajakutana naye na anamkaribisha ofisini kwake kueleza ukweli wa yote yanayosikika na asipofanya hivyo taratibu za chama zitafuatwa.

Bashiru alisema wapo wana CCM waliokuwa wanagombea nafasi mbalimbali ili tu wapate kuongoza na si kukiimarisha chama hicho na kufanya hivyo wamekiuka kanuni zinazo mtaka kila mwanchama awe kiongozi mahiri, muadilifu, mchapakazi na mzalendo.

“Nasema hivi, chini ya uongozi thabiti wa Rais Magufuli, mimi na Kamati Kuu ya CCM, viongozi wote wanaoutaka urais kwa sasa wakome, wakatafute urais nje ya chama chetu,” alisema.

Bashiru alisema hajawahi kumsikia Membe akifanya shughuli zozote za chama tangu aliposhindwa kuchaguliwa na chama hicho kuwa mgombea wa urais wa mwaka 2015.

“Iweje anafanya vikao vya chini chini vya kuusaka urais na kumpiku Rais Magufuli? Njoo mezani tujenge hoja na asipokuja tutaanza kuamini kuwa hana nia nzuri na hapo ndipo taratibu za chama zitaanza kufanyika,” alisema.

ANDIKO LA MEMBE

Baada ya kauli hiyo, juzi usiku kulisambaa andiko ambalo MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Membe ili athibitishe kama ni kweli kaliandika lakini hakupatikana baada ya kudaiwa yuko nje ya nchi na badala yake watu wake wa karibu walithibitisha kuwa limeandikwa na mwanasiasa huyo.

Kupitia andiko hilo, Membe, aliyewahi pia kuwa Mbunge wa Mtama alisema amepokea wito wa Bashiru na atakwenda kumwona.

Pia alisema alishangazwa na namna utaratibu wa wito huo ulivyotumika.

“Kutokana na taarifa za katika mitandao jioni hii (juzi) na ujumbe mwingi unaokuja kwangu, nimeamua kutoa ujumbe huu kwa wote wanaonitakia mema,” lilisema andiko hilo na kuongeza:

“Usiku huu nimempelekea KM (Katibu Mkuu) wa chama chetu, Bashiru, ujumbe wa kukubali kumwona mara nitakaporejea kutoka nje ya nchi. “Nimeshangazwa kidogo na utaratibu uliotumika kuniita, lakini kwa sababu ya ugeni kazini na kwa sababu ninamheshimu, nitakwenda kumwona ofisini kwake.”

Pia kupitia andiko hilo, Membe, alimwomba Bashiru kuwa siku atakayokwenda kumwona awepo pia Musiba ili atoe ushahidi kwa madai kuwa ndiye aliyeanzisha suala hilo.

“Wote tunajua kuwa mwanzilishi wa tuhuma zote dhidi yangu tunazozisoma na kuzisikia katika chombo cha habari na mitandaoni ni Musiba.

“Nimemwomba Bashiru, siku nitakayokwenda kumwona, Musiba awepo ili atoe ushahidi kwa sababu mtoa tuhuma ndiye mwenye wajibu wa kuthibitisha aliyoyasema. Mimi kama mtuhumiwa siwajibiki kufanya hivyo. Burden of proof ni ya Musiba. Mimi nitajibu mapigo atakapomaliza kutoa ushahidi mbele ya KM,” ilieleza sehemu ya andiko hilo.

Pia andiko hilo lilisema kuwa alimweleza Bashiru kuwa alitegemea baada ya tuhuma hizo kwa watu na viongozi wenye historia na heshima kama yeye, mtoa habari huyo angehojiwa ili athibitishe madai yake na aonywe.

Mbali na hayo, lilisema kuwa baada ya kujiridhisha kuwa aliyoyasema Musiba yana mashiko, kamati ya maadili ya chama hicho ingefanya kazi ya kuwaita wahusika kwa kanuni na taratibu za chama kuwahoji.

“Kutokufanya hivyo, nimemwambia KM (Katibu Mkuu) ndiko kulikotufanya wengine tuanze kuamini kuwa sauti tunayoisikia ni yake Musiba, lakini akili si yake ni ya kupewa na waliomtuma, wanaomlipa na wanaomlinda. Tuhuma nitungiwe mimi, halafu nitakiwe kuzijibu. Nikaamua kumpuuza na nitaendelea kufanya hivyo. Kumjibu Musiba ni kumpa heshima asiyostahili.

“Hadi hapo nitakapokutana na KM wa chama chetu na Musiba, tuvute subira! Nawapenda na kuwashukuruni wote mliotaka niseme neno. BM,” lilisema andiko hilo.

 WANACHAMA WALIOFUKUZWA

Kuhusu wanachama waliofukuzwa, Bashiru, aliwataka kuomba msamaha ili waendelee kukijenga chama.

“Hatuwezi kuendelea na hali ya kutoaminiana ndani ya CCM, ninamtumia salamu Mkuu wa Wilaya ya Kilombero kujirekebisha kwa sababu hafanyi ziara wilayani mwake wala shughuli zozote za maendelelo anakaa tu, vilevile onyo kwa wakuu wote wa wilaya, kila mmoja awajibike katika nafasi yake katika kufanya shughuli za maendelelo,” alisema.

Pia aliwaonya viongozi walio madarakani katika mikoa yote kuacha tabia ya kuwanyanyasa na kuwakalia vichwani wakuu wa wilaya kwa madai kuwa wao ndiyo wenye mamlaka makubwa zaidi.

“Nimesikia wapo baadhi ya viongozi wa CCM wanawakalia vichwani viongozi wa Serikali katika wilaya au mikoa yao kwa madai kuwa wao ndio viongozi wa chama kilicho madarakani, tusiwaruhusu kufanya hayo badala yake washirikiane ili kutatua changamoto za maendeleo,” alisema.

 WAKUU WA MIKOA

Pia aliwaonya wakuu wa mikoa wanaotumia madaraka yao vibaya hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema hakupenda mgogoro uliokuwapo mwezi uliopita miongoni mwa madiwani na wabunge wa Geita kuhusu wapi ijengwe hospitali ya rufaa kati ya Nzera na Katoro.

“Hongera kwako mkuu wa mkoa na watendaji wako kwa kujadiliana na kufikia muafaka kwa sababu unaweza kugawanya chama, mmenusurika, ningewashughulikia hapa hapa,” alisema.

Mgogoro huo uliowagawa wabunge katika makundi mawili ulinguruma kwa miezi kadhaa na kuleta mtafaruku huku kila upande ukitoa sababu za umuhimu wa hospitali kupewa hadhi ya kuwa ya wilaya.

Baada ya mgogoro huo, walikubaliana na kufikia uamuzi wa kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Nzera kuwa Hospitali ya Wilaya kwa kuwa eneo hilo liko pembezoni na lina idadi kubwa ya watu.

“Wakuu wa mikoa na wabunge waache kumdhalilisha Rais kwa sababu yeye ndiye aliyewapa dhamana ya kuongoza na badala yake watumie rasilimali zilizopo mikoani mwao kwa kuzifanyia miradi ya maendeleo, waache fujo kwa sababu wote wako katika 18 yangu, siwatishi lakini waache chama kifanye kazi yake,” alisema.

 

TAASISI ZA CCM KUDORORA

 

Alisema taasisi nyingi za chama hicho zimedorora kutokana na ubinafsi miongoni mwa baadhi ya viongozi.

“Tasisi kama Jumuiya ya Wazazi ambayo ipo kama mgonjwa aliyekuwa mahututi, na nyingine ni Umoja wa Vijana nayo iko hoi na kwa upande wa Umoja wa Wanawake kidogo wanajitahidi, hivyo hakikisheni tunatoka katika hali hiyo kwa sababu iwapo mtaweka mikakati mizuri ya kuendeleza miradi ya taasisi na kuwa na uongozi mzuri nina uhakika tutatoka hapa tulipo,” alisema.

Jana aliendelea na ziara mkoani hapa kwa kuzungumza na watendaji wa CCM pia alitembelea miradi mbalimbali ili kujionea utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,340FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles