26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Jaji awa ‘mbogo’ kesi ya Mbowe, Matiko

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM


JAJI Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ameamuru mwenendo wa kesi namba 212/2018 na uamuzi uliomfutia dhamana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, umfikie ofisini kwake ndani ya saa moja.

Jaji Rumanyika alifikia uamuzi huo jana saa sita mchana akitaka hadi saa saba nyaraka hizo ziwe zimeshamfikia na mawakili wazipate.

Hayo yaliibuka  baada ya kupitia jalada lililomfikia na kubainika kwamba mwenendo wa kesi na uamuzi huo haukuwepo.

“Nani mwenye simu ya hakimu anayesikiliza kesi hii…. Nani mwenye namba ya simu ya in charge Kisutu….  “alihoji Jaji Rumanyika bila majibu ndipo Wakili Peter Kibatala, anayemwakilisha Mbowe na Matiko, alipotaja namba ya karani wa Hakimu Wilbard Mashauri.

Jaji alisema juzi aliaminishwa kwamba jalada hilo lilishakamilika na limeshafika ndio sababu alipanga kusikiliza rufaa hiyo jana.

Kibatala alitaja namba za Karani Cosmas na alipomaliza kuitaja Jaji aliinua simu yake ya kiganjani akampigia.

Jaji : Naitwa Rumanyika.

Cosmas :Nani..

Jaji :Rumanyika hapa Mahakama Kuu.

Cosmas :Ahaaa.

Jaji :Unafahamu kesi namba 112 /2018.

Cosmas :Ndio.

Jaji:Wahusika kina nani.

Cosmas : Mbowe na wenzake.

Jaji :Kumbukumbu hazijakamilika.. Nakala ya uamuzi na mwenendo wa kesi havipo.

Cosmas : Havijamalizika kuchapwa wakati jalada likiondoka jana.

Jaji:Niletee hizo, ziwe zimechapwa au zimeandikwa kwa mkono.. Niletee nakusubiri ofisini chumba namba 16.

Baada ya kumaliza kuwasiliana na karani huyo, aliagiza rufaa hiyo isikilizwe leo saa mbili asubuhi baada ya pande zote kupata nakala zinazohitajika.

Awali Wakili Kibatala alikuwa tayari kuendelea na kesi lakini Jamhuri ikiongozwa na Faraja Muhimbi, waliomba iahirishwe sababu hawakuwa na nyaraka hizo za mahakama.

Jaji Rumanyika alisema yuko tayari kuanza kusikiliza hata saa kumi jioni kutokana na dharura ya rufaa hiyo.

“Hii ni dharura tukubaliane kwenda nayo hivyo hivyo, mwenendo kama umeandikwa kwa mkono twende nao hivyo hivyo, asiyeelewa aje kuniuliza,” alisema.

Jaji Rumanyika aliutaka upande wa Jamhuri kufika na majibu leo wakieleza kama kiapo kilichowasilishwa Mahakama ya Kisutu na upande wa Jamhuri, kilichoapwa na Kamanda wa Polisi Ilala, Salum Hamduni, kikionesha washtakiwa wanakaidi amri ya mahakama na kama washtakiwa walipewa nafasi ya kukijibu kiapo hicho.

Pia alitaka waeleze madhara ya amri ya mahakama kuhusu dhamana isimamiwe na polisi. Hata hivyo washtakiwa hao hawakuwahi kuwasilisha kiapo kinzani wakijibu kiapo cha Hamduni.

Mahakama inatarajia kusikiliza rufaa hiyo namba 344/2018 leo asubuhi.

Mbowe katika utetezi wake ili asifutiwe dhamana alidai kuwa Novemba 2,  alikwenda nchini Ubeligiji wakati akisubiri ahadi ya kuonana na daktari wake Novemba 8 na kwamba alishauriwa asisafiri mwendo mrefu akiwa angani.

Kwa upande wa Matiko akijitetea alidai kuwa  alishindwa kufika mahakamani kwa sababu alihudhuria mkutano wa michezo kwa mabunge ya Afrika Mashariki akiiwakilisha Tanzania.

Katika uamuzi wake Hakimu Mashauri alisema kwamba sababu zilizotolewa na utetezi zote hazina mashiko na kwamba pamoja na nyadhifa walizonazo, lakini ni watuhumiwa wa makosa ya jinai mahakamani hapo.

“Nchi yetu inaendeshwa kwa matakwa ya sheria, pamoja na nyadhifa walizonazo mshtakiwa wa kwanza na wa pili, wanakabiliwa na makosa ya jinai wanapaswa kutii amri za kisheria” alisema Hakimu na kuongeza.

“Kwa kuwa mshtakiwa wa kwanza taarifa zake zinakinzana, hati yake ya kusafiria inatofautiana na maelezo yake, mshtakiwa wa tano pia sababu zake hazina mashiko, mahakama yangu inawafutia dhamana kuanzia leo” alisema Hakimu Mashauri na kuwafutia dhamana.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine wanaoshtakiwa nao katika kesi ya jinai namba 112  ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles