24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Rushwa ya ngono yatikisa UDSM

Na EVANS MAGEGE


TUHUMA za rushwa ya ngono zilizotolewa juzi na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Vicensia Shule, kupitia akaunti yake ya mtandao wa twitter, zimeonekana kutikisa taasisi hiyo ambapo jana kamati yake ya nidhamu ilikutana kuanza kuchunguza kashfa hiyo.

Katika akaunti yake ya twitter Dk. Shule juzi alindika;  “Baba MagufuliJP (Rais John Magufuli) umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM. Nilitamani nikupokee kwa bango langu ila ulinzi wako umenifanya ninyamae. Nasubiri kusikia toka kwako maana naamini wateule wako ni waadilifu watakwambia ukweli”.

Mtanzania ilipomtafuta, Dk. Shule alisema ujumbe huo ni wake na ameamua kuandika suala hilo kwa sababu limekuwapo chuoni hapo kwa muda mrefu.

Alisema kwa nafasi yake ameripoti tatizo hilo mara kadhaa kwenye vikao vya menejimenti lakini mpaka sasa hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa ili kukomesha vitendo hivyo.

“Msimamo wetu tumekuwa tunasema kwamba ushahidi wa haya masuala ni kwamba yanaripotiwa, kwa hiyo chuo kiunde mfumo, sio kuunda tume ya kuchunguza na kuondoka, kuweka na mfumo ambao ni endelevu kuhakikisha suala hili halitokei.

“Kwenye vikao vya menejimenti wanasema nilete ushahidi,  ujue ni ngumu sana mtoto ambaye amebakwa alafu kaja kuniambia kwa siri yaliyomkuta, leo umpeleke kwenye menejimenti kwa ushahidi, ni ushahidi upi wanautaka zaidi ya taarifa za matukio haya yanayotokea mara kwa mara?,’ alihoji Dk. Shule.

Alikwenda mbali kwa kusema kwamba wanafunzi wengi wanaofikisha malalamiko ni wale wa shahada ya uzamili na hivyo hajui tatizo ni kubwa kiasi gani kwa wale wa shahada za chini ambao ni waoga kujieleza.

“Tujiulize tatizo ni kubwa kiasi gani kwa hawa watoto wa dogo wanaoingia mwaka wa kwanza,  hatujui kwa wale wa mwaka wa pili na watatu ndio maana ninachokitaka mimi ni chuo kuweka mfumo endelevu wa kuwafanya hawa waathiriwa kupaza sauti yao.

“Rushwa ni vita  na chuo kitambue rushwa ya ngono ni vita kweli kweli kama ilivyo rushwa ya fedha,” alisema Dk. Shule.

MAKAMU MKUU WA CHUO (VC)

Baada ya maelezo hayo ya Dk. Shule, gazeti hili lilizungumza na Makamu Mkuu wa UDSM,  Profesa William Anangisye, ambaye alisema licha ya Dk. Shule kuandika tuhuma hizo kwenye mitandao ya kijamii, hajawahi kuzifikisha ofisini kwake.

Alisema inawezekana chuoni hapo kuna matatizo mengi lakini tangu apewe jukumu la kukiongoza chuo hicho, hajawahi kufikishiwa tuhuma za rushwa ya ngono.

Kwa mukutadha huo alimtaka mwandishi arudi kumuuliza Dk. Shule maswali manne ambayo yeye alihoji.

Maswali hayo ni moja,  kwa nini hajawahi kuwasilisha tuhuma hizo ofsini kwa Makamu Mkuu wa Chuo?

Pili, kama Dk. Shule amewahi kufikisha taarifa hiyo kwenye menejimenti, afafanue ni menejimenti ipi, ya idara, college au chuo?

Tatu, Dk. Shule ni kiongozi ndani Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDASA) je suala hilo amewahi kulifikisha kwenye vikao vya jumuiya hiyo?

Nne,  kama tatizo hilo ni la muda mrefu kwa nini asubiri ujio wa Rais Dk. Magufuli  ndio aliwasilishe kwa njia ya mitandao ya kijamii?

Baada ya maswali hayo kwa Dk. Shule, Profesa Anangisye alisema yeye ana shahada ya uzamivu katika masuala ya uadilifu wa walimu hivyo anaamini kuwa ni wajibu wa mwalimu kulinda mwanafunzi.

“Na mimi nikimshika mtu nikapata ushahidi, taratibu za ualimu haziruhusu mtu wa aina hii kuendelea kuwa mwalimu na sio taratibu tu hata taratibu pia za nchi. Kwa hiyo pale atakapoonekana kwamba ni mwalimu hatutafumbia macho,” alisema Profesa Anangisye.

MAJIBU YA DK. SHULE

Mwandishi alirudi tena kwa Dk Shule kama alivyohoji Profesa  Anangisye, ambapo  Dk. Shule alijibu kwa ujumla akimtaka kiongozi huyo wa chuo awaulize wasaidizi wake ( Depute Vice Chancellors-(DVCs)

“Awaulize wasaidizi wake ni mara ngapi nimekutana nao kuwaelezea suala hili?,” alihoji Dk. Shule.

Dk Shule akizungumzia nafasi yake ya uongozi wa  UDASA na hatua alizochukua kuliwasilisha suala hilo ndani  jumuiya hiyo, alisema mara nyingi uongozi wa jumuiya hiyo umeshindwa kukutana kufanya vikao kwa sababu ya Makamu Mkuu wa Chuo kuwazuia kuitisha mikutano na kuwanyima ukumbi wa kufanyia mikutano yao.

Akijibu swali la kwanini amesubiri ujio wa Rais Dk. Magufuli ndio akaripoti tuhuma hizo kwenye mitandao ya kijamii, Dk. Shule alisema. “Ninayo haki ya msingi ya kikatiba kufanya hivyo kama mwananchi,” alisema.

Alisema yeye kuwa mtumishi wa umma sio sababu ya kuangusha haki yake ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza.

MAKAMU WA CHUO TENA

Baada ya maelezo ya Dk. Shule, gazeti hili lilirudi kwa mara nyingine kwa Profesa Anangisye na kumweleza alichosema Dk Shule.

Profesa Anangisye aliendelea kuhoji kama Dk. Shule aliripoti taarifa hizo kwenye menejimenti na kwamba wasaidizi wake (DVC) wanajua na kama aliona mambo hayaendi kwa nini asingefika ofisini kwake kumtaarifu?

Alisema UDASA ina kamati ya utendaji kwa nini hajawahi kutoa taarifa hizo?

“Waliomba ukumbi na tulipozuia hapajawahi kuwa na kikao chenye agenda ya suala la ngono. Angenda zote za UDASA hupitishwa na kamati tendaji na yeye ni mjumbe sijawahi kuona hoja kama hiyo anayotuhumu,” alisema Profesa Anangisye.

Alisema UDSM inawalimu zaidi ya 1200  inawezekana watuhumiwa ni watu 10 au 20 hivyo kusitumike madai hayo kuchafua walimu wote.

Alisema Dk. Shule anatakiwa atoe takwimu za kutosha za wanafunzi walioathiriwa kwa ngono pamoja na ushahidi.

Baada ya mazungumzo hayo,  Profesa Anangisye alimpigia tena simu mwandishi na kumwambia kwamba anamsifu Dk. Shule kwa ujasiri aliouchukua.

“Hii ni alamu ya kuniamsha pia, kweli suala hili linafanyiwa kazi lakini alichokifanya kinaonyesha kuwa angalau kuna watu majasiri, amediriki kusema ukweli kama upo na kama haupo waja.

“Kwangu mimi namshukuru Mungu kwamba angalau nimempata mtu ambaye atanisaidia kupata data. Sema tu kama nilivyosema mwanzoni hajawahi kuja ofsini kwangu kunieleza jambo kama hili,” Profesa Anangisye.

MWENYEKITI  UDASA

Kwa upande wake mwenyekiti wa UDASA, Dk. George Kahangwa, alisema  Dk. Shule hajawahi kumpa taarifa hiyo.

Dk. Kahangwa alikwenda mbali kwa kusema kitendo cha Dk. Shule kutoa habari hiyo kwenye mitandao ya kijamii kimekiuka taratibu nyingi.

Alisema UDSM  ina sera ya Anti-Sexual Harassment ambayo inaeleza utaratibu wa kufuata kunapotokea jambo kama hilo na inaeleza wanaohusika na jambo hilo wanaweza kuchukuliwa hatua gani.

Alisema katika  idara kuna watu wanaoitwa ‘gender focal point’ ambao wanawajibu wa kushughulikia masuala hayo .

“Ndani ya UDASA , Dk Shule hajalileta suala hilo, lilivyoanza kusambaa jambo hili ndio tukaanza kuhoji kulikoni, hata mimi mwenyewe niliwasiliana naye nikamwambia anipe taarifa alizodai anazo, alichonijibu alisema kuwa anadhani hili ni zaidi ya UDASA , akasema anatunza siri ya wale waathirika wa hilo jambo.

“Sasa inakanganya amesema anatunza siri ya waathiriwa lakini bado anatawanya habari  bila kuweka ushahidi mezani wala ujasiri wa kufuata njia sahihi,” alisema Dk. Kahangwa

DVC

Gazeti hili lilimuuliza Msaidizi wa Makamu Mkuu wa Chuo cha UDSM kitengo cha taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa, ambaye alijibu yuko Songea hivyo hawezi kuzungumzia jambo ambalo halijui.

Alipotafutwa Msaidizi wa Makamu Mkuu wa Chuo cha UDSM kitengo cha utafiti, Profesa Casbert Kinambo alisema kama Dk. Shule amewahi kuwasilisha ofsini kwake basi suala hilo linafanyiwa kazi lakini taarifa hizo hazijawahi kumfikia.

Alipotafutwa Msaidizi wa Makamu Mkuu wa Chuo cha UDSM kitengo cha Utawala, Profesa David Mfinanga alisema yupo kwenye kikao hivyo hakuwa na nafasi ya kuzungumza lolote.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles