30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JPM, Mbeki wateta kubana watakatishaji fedha haramu

Na MWANDISHI WETU


RAIS Dk. John Magufuli, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ambaye pia ni Mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu lililoundwa na Umoja wa Afrika (AU), kushughulikia tatizo la utakatishaji wa fedha.

Viongozi hao walikutana Ikulu jijini Dar es Salaam jana, ambapo Mbeki, alisema mazungumzo hayo yamemwezesha kupata taarifa na uzoefu muhimu kutoka kwa Rais Magufuli kuhusu juhudi zinazofanywa na Tanzania kukabiliana na utoroshaji wa fedha katika maeneo mbalimbali yakiwemo sekta ya madini na rushwa, matatizo ambayo yanazikabili nchi zingine za Afrika.

“Ni wazi kwamba juhudi zinazofanywa na Tanzania zina umuhimu mkubwa kufanywa na nchi zingine za Afrika, kwa pamoja Waafrika tunaweza kukabiliana na utoroshaji wa fedha zetu kwenda nje ya nchi zetu na Rais Magufuli amezungumza kwa usahihi kabisa juu ya matrilioni ya dola za Marekani zinazopotea kupitia utoroshaji huo,”  alisema Mbeki.

Kwa upande wake Rais Magufuli, alimpongeza Mbeki kwa kuongoza jopo hilo na kubainisha kuwa Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano utakaowezesha kunusuru rasilimali za Afrika, hivyo amemshauri kutenga muda wa kutosha ili apate taarifa za uhakika kutoka kwa viongozi na wataalamu katika mamlaka zinazodhibiti utoroshaji wa fedha hapa nchini.

Ripoti ya taasisi ya kimataifa ya Global Financial Intergrity (GFI) ya mwaka 2014 kuhusu tatizo la utoroshaji wa fedha za Afrika inasema Afrika inapoteza Dola za Marekani kati ya trilioni 1.4 na trilioni 2.5 kwa mwaka kutokana na tatizo hilo.

Kutokana na hali hiyo kwa ujumla Afrika imepoteza Dola za Marekani Trilioni 95 kwa miaka 50 iliyopita, ikiwemo Tanzania iliyoripotiwa kupoteza dola za Marekani Bilioni 19 katika miaka 40 iliyopita.

“Njia nyingi zinazotumika katika kutupotezea hizo fedha na kuibiwa, wanaweza wakaja kuwekeza lakini kila siku wakawa wanasema wanapata hasara kumbe hawapati hasara, wanatengeneza faida kubwa lakini kwenye vitabu wanawaandikia wanapata hasara, wanaweza wakaja kama wawekezaji na wakawa wanazidisha gharama za uwekezaji kuliko uhalisia,”  alisema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Nicolai Astrup, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumshukuru kwa mchango mkubwa ambao unatolewa na nchi yake kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali zikiwemo elimu, kilimo, nishati na gesi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles