NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Hans Van der Pluijm, amesema hafikirii kuwa kupata mabao mengi katika mechi ndiyo kufanya vizuri, yeye anachokiangalia na kukiamini katika kikosi chake ni ubora, hata kama watashinda moja kila mechi.
Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi uliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Pluijm alisema furaha yake ni kuona kikosi chake kikiingia uwanjani na kufanya vizuri hata wakipata idadi ndogo ya mabao lakini kimeonyesha ubora huo ni ushindi tosha.
“Ninachokipa kipaumbele kwangu ni kiwango cha soka wanachoonyesha wachezaji wangu uwanjani, sifikirii kuwa kupata mabao mengi ndiyo kufanya vizuri au kuwa na kikosi bora.
“Nitafurahi kama tutashinda kila mechi, siyo lazima tupate mabao mengi ndiyo watu waone tumefanya kitu uwanjani,” alisema Pluijm.
Yanga imejikita kileleni mwa ligi ikiwa na pointi sita, sawa na Azam FC, Simba, Mtibwa Sugar na Majimaji, ambapo timu hizo zinatofautiana kwa idadi ya mabao.
Kikosi hicho kilianza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa kwanza msimu huu, ambapo katika mechi inayofuata itavaana na JKT Ruvu Uwanja wa Taifa.