24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kipindupindu chaota mizizi Dar

Pg 3 sept 18TUNU NASSOR NA HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAM

UGONJWA wa kipindupindu umeendelea kuota mizizi jijini Dar es Salaam, baada ya kuzidi kuenea na kufanya idadi ya watu waliougua hadi sasa kufikia 1,458.

Kati ya wagonjwa hao, waliopoteza maisha wamefika 18, huku wagonjwa wapya ambao wameripotiwa kati ya juzi na jana, wamefika 61.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, maofisa wa afya wa wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala, walisema wagonjwa wapya walioripotiwa kuanzia juzi saa 10 jioni hadi jana saa 6 mchana, Kinondoni walikuwa 16, Ilala 27 na Temeke 6.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Aziz Msuya, alisema wagonjwa 857 wamefikishwa Kituo cha Mburahati tangu ugonjwa huo uripotiwe.

Alisema kati ya wagonjwa hao, waliopoteza maisha wamefika wanane.

Dk. Msuya alisema maeneo yanayoongoza kwa kutoa wagonjwa wengi ni Kata ya Manzese, Tandale na Kigogo.

Alisema jitihada mbalimbali zinafanyika ili kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kufanya msako wa kukamata kwa wafanyabiashara wanaouza vyakula usiku katika mazingira yaliyopigwa marufuku.

Dk. Msuya alisema wameendelea kutoa elimu kwa wananchi, na tayari wamewafikia watu 8,465 na kuwashauri kufuata kanuni za afya.

“Tumefanya uchunguzi wa kimaabara na kubaini dawa iliyokuwa inatumika awali ambayo ni ‘ Erythromycin’, haikuwa ikiwaua wadudu wa ugonjwa huo, ambao ni ‘Vibro Cholera Ogawa’ na sasa wamegundua dawa sahihi ya kutibu ugonjwa huo,” alisema Dk. Msuya.

Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Victorina Ludovick, alisema idadi ya wagonjwa 480 wamefikishwa Kituo cha Buguruni na waliothibitishwa kufariki dunia ni 10.

Alisema maeneo yaliyoathirika zaidi ni Buguruni, Vingunguti na maeneo ya pembezoni mwa Mto Msimbazi (Mchikichini).

“Chanzo kikubwa cha ugonjwa huu ni maji yanayotoka katika visima vifupi ambavyo vimechimbwa bila kufuata utaratibu wa afya, tunashirikiana na mamlaka nyingine kufukia visima vyao.

“Changamoto inayotukabili ni ubutu wa sheria kwa kuwa faini zinazotozwa ni sh 50,000 hivyo watu hao huona ndogo na kulipa kisha kurudia tena,” alisema Dk. Victorina.

Naye Ofisa Afya wa Manispaa ya Temeke, William Muhemu, alisema wamepokea wagonjwa wapya sita, kati yao wanawake watatu na wanaume watatu.

“Idadi ya wagonjwa waliofikishwa katika kambi za manispaa hii ni 121,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles