Nora Damian, Mtwara
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Glasius Byakanwa, amesema Sospa ilitungwa kwa jazba na mihemko ya wanaharakati kwa sababu haimfanyi mtoto wa kike awajibike.
Aidha, amesema suala la mimba za utotoni bado ni changamoto kubwa mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Novemba 18, amesema changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na udhaifu uliopo katika Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (Sospa 1998) ambayo amedai haimfanyi mtoto wa kike awajibike.
“Sospa ilitungwa kwa jazba na mihemko ya wanaharakati. Najua wanaharakati wa jinsia wanaweza wakachukia lakini mimi ni baba wa watoto wa kike pia nataka watoto wa kike wawe responsible (wawajibike),” amesema Byakanwa.
Amesema suala la mimba za utotoni linahitaji tafakari kubwa na kwamba kuendelea kumuadhibu mwanamume kutamfanya mtoto wa kike asiwajibike kwa kujizuia.
“Unamfunga mwanamume miaka 30 maana yake unaruhusu mtoto atakayezaliwa akue hana mzazi,” amesema.