27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Majina hewa yabainika malipo ya korosho

Na NORA DAMIAN-MTWARA


KAZI ya uhakiki wa majina ya wakulima wa korosho imeanza huku majina hewa yakibainika, likiwamo la mwenza wa karani wa chama cha msingi.

Katika uhakiki huo ambao unafanyika usiku na mchana kwa ajili ya malipo ya wakulima, yamebainika majina matatu katika Chama cha Msingi cha Makonga   wilayani Newala.

Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya ya Newala, Aziza Mangosongo, alisema walibaini   majina hayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi.

Alisema mmoja wa makarani wa Makonga (jina linahifadhiwa),  aliandika malipo hewa kwa jina la mpenzi wake (jina linahifadhiwa).

“Kutokana na uhusiano wao wa  mapenzi ameamua kumuandikia malipo hewa na kuna wengine wameandika ndugu zao.

“Tumekamata kilo 200 ambazo zimeandikwa malipo hewa, kama hali ndiyo hii kwa makarani wengine ikoje?

“Tunawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano, wajumbe wa bodi, wenyeviti na makatibu wa Amcos zote wawe makini na waandike kile ambacho ni sahihi,” alisema Mangosongo.

Alisema karani huyo na wote waliohusika kuandika majina hewa wanaendelea kuhojiwa na utafanyika  uhakiki katika kila shamba la mkulima na kujiridhisha na korosho alizowasilisha.

“Mtu hana shamba lakini unakuta jina lipo na akaunti namba, tukiwagundua wengine tutakula nao sahani moja” alisema.

UHAKIKI MASHAMBANI

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, alisema kabla ya kulipwa kila mkulima atatakiwa kuonyesha shamba lake na kama hana ataeleza korosho amezipata wapi.

“Watendaji wa vyama vya msingi ambao hawana mashamba wametengeneza majina hewa.

“Unakuta mtendaji alikopeshwa Sh milioni 200 na chama cha msingi lakini hana shamba, anakusanya korosho za wakulima halafu anaandika risiti hewa,” alisema Byakanwa.

Mkuu huyo wa mkoa pia aliibua ufisadi katika   korosho ambao ulikuwa ukifanywa kwa ushirikiano wa waendesha maghala, wasafirishaji na wabanguaji.

Alisema baadhi ya wasimamizi wa maghala wamekuwa wakisema korosho zimepotea lakini cha kushangaza hawatoi taarifa polisi.

Alisema  katika ghala la Micronix wilayani Newala, mwaka jana zilipotea tani 200 za korosho.

“Wanachosema mwendesha ghala atamuarifu mwenye mali na atapaswa kulipia mzigo kulingana na bei ya soko.

“Wanatengeneza upotevu halafu bei ikiwa kubwa wanakuja kuziuza. Mwendesha ghala anasema yuko tayari kulipa akiulizwa ulikwenda polisi hapana, polisi hakuna ripoti ya ghala kuvunjwa, kuvamiwa au kuungua moto.

“Wanasema korosho imepotea kwa sababu ya unyaufu wakati kitaalam baada ya miezi sita ndiyo inaweza kupotea na kiwango cha upotevu ni asilimia 0.5,” alisema.

Alisema hadi sasa kuna wakulima kutoka Chama cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU)  ambao bado wanadai fedha kutokana na korosho zao kupotea katika msimu wa 2017/2018.

Kuhusu viwanda, alisema kati ya sita vilivyobinafsishwa ni viwili tu vya Micronix (Mtwara) na Micronix (Newala ndivyo vinazalisha tani 10,000 kwa mwaka.

“Vingi havipo kama viwanda, kama Agro Focus na Olam vilivyopo Mtwara havizalishi. Mashine zilishang’olewa na sasa vinatumika kama maghala,” alisema.

Hata hivyo alisema tayari maofisa kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina wako mkoani hapa wakiendelea na tathmini ya viwanda hivyo.

KAULI YA WAZIRI

Juzi, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema wakulima 2,168 kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wamelipwa Sh bilioni mbili baada ya kuuza korosho.

Wakulima hao ni miongoni mwa waliohakikiwa kutoka vyama vya msingi 35 kati ya 50 ambavyo Serikali imeanza navyo.

Pia korosho za magendo zimeendelea kukamatwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mtwara.

Waziri Hasunga, alisema hadi Ijumaa ya wiki iliyopita tani 118,700 zilikusanywa kutoka maghala ya vyama vya msingi.

“Tumeipa uzito mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa sababu ndiyo inazalisha kwa kiwango kikubwa, tumeshawalipa wakukima 2,168 na mpango huo unaendelea kwa vyama vilivyohakikiwa.

“Malipo yataendelea kufanyika sambamba na kazi nyingine kwa sababu hali ya hewa inabadilika na kuna dalili za mvua kuanza. Tutahakikisha hadi Ijumaa ijayo korosho ambayo iko tayari wananchi wawe wamelipwa fedha zao,” alisema Hasunga.

Pia alisema kwa sasa maghala mengi hayapokei korosho kutoka katika vyama vya msingi kwa sababu hakuna sehemu ya kuweka.

“Wakati wowote kuanzia sasa zitaanza kusafirishwa na kupelekwa kwenye maghala mengine  kutoa nafasi yaendelee kupokea korosho,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles