32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu: Maonyesho ya viwanda, biashara na madini yanapaswa kuigwa na Mikoa mingine

Anna Potinus



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema maonyesho ya viwanda vidogo na biashara ndogo ndogo na yale ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini yanayofanyika nchini ni ubunifu muhimu na hauna budi kuigwa na mikoa mingine kama ilivyofanywa na Pwani, Geita na Simiyu.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 16, wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge mjini Dodoma, ambapo amesema maonyesho hayo yanahamasisha wananchi wengi zaidi washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda.

“Ubunifu huu wa kufanya maonesho ya viwanda ya kimkoa, kikanda na kitaifa ni jambo muhimu sana. Maonyesho haya, yanatupa fursa ya kujitangaza na kutathmini hatua tuliyofikia katika utekelezaji wa ajenda ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kubaini changamoto zilizopo.

“Napenda kuielekeza mikoa mingine iige mifano hiyo ya mikoa ya Pwani, Simiyu na Geita ili kuhamasisha wananchi na wadau wengine washiriki ipasavyo katika ujenzi wa viwanda na kuleta teknolojia mpya za viwanda na sekta ya madini,” amesema.

Aidha, amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji na kwamba hatua stahiki hazina budi kuchukuliwa ili kudhibiti hali hiyo isiendelee.

“Miradi mingi ya maji nchini imekwama au kutoleta tija kutokana na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Hivyo, niwasihi Wabunge wenzangu muwahamasishe wananchi na wadau kutoa maoni yatakayosaidia kujenga na kuboresha vema sheria zinazokusudiwa kulinda mazingira yetu pamoja na vyanzo vya maji,” amesema Waziri Mkuu, na Bunge limeahirishwa hadi Januari 29, mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles