Asifiwe George na Ester Mnyika, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kutumia vibaya mitandao ya kijamii kufanya uhalifu wa kutengeneza habari za uongo na uzushi dhidi ya viongozi au watu maarufu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova alisema watu hao wamekuwa wakitumia vibaya majina ya watu maarufu hasa wanasiasa.
Kova alitaja majina ya wanasiasa yanayotumiwa vibaya kuwa ni mgombea ubunge Jimbo la Kibamba, John Mnyika na mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Aliwataja watuhumiwa hao, kuwa ni Joel Lumbay (32), Omar Suleiman wote wakazi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Michael Nickson (32) mkazi wa Tegeta, Patrick Natala na Maxmillian Msacky wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Alisema watu hao, wamekuwa wakituma ujumbe mbalimbali wakionesha viongozi hao walikuwa wanajadili jambo fulani dhidi ya kundi au chama kingine cha siasa kwa kutumia mitandao.
“Wana tabia ya kutengeneza ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwa lugha iliyozoeleka kama ‘kuchati,’ lakini mawasiliano hayo hayapo… yanakuwa yametengenezwa ili kutimiza malengo yao. Jambo hili ni kosa la jinai na linaweza kuchochea chuki katika makundi ya watu,” alisema Kova.
Alisema jeshi hilo linaendelea kuwasaka watu hao kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Kiongozi au mtu yeyote atakayeona ameathirika na mbinu chafu za kihalifu asisite kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe mara moja,” alisema.