NYOTA wa zamani wa klabu ya Barcelona ambaye kwa sasa anakipiga klabu ya Al Sadd, Xavi Hernandez, ameanza vizuri katika klabu hiyo mpya baada ya kutoa pasi za mwisho katika mchezo wa Ligi dhidi ya Al-Mesaimeer.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu nchini Qatar, Xavi alitoa mchango mkubwa wa kuongeza mashambulizi huku akitoa pasi ya mwisho na klabu yake ikishinda mabao 4-0.
Hata hivyo, mchezaji huyo alishangaa kuona mashabiki wachache ambao walijitokeza katika uwanja huo ambao ulichukua watazamaji 2,254, huku akizoea kuona watazamaji wengi kwenye Uwanja wa Nou Camp ambao unachukua zaidi ya watu 99,354.
Mchezaji huyo alitumia dakika 12 tangu alipoingia uwanjani na kupiga pasi iliyowafanya wapate bao la kwanza.
Hata hivyo, mchezaji huyo kutokana nchini Hispania, amesisitiza kuwa anafurahia maisha ya soka ya nchini Qatar.
“Nimekuwa na furaha kubwa kucheza soka nchini hapa, ninaamini nitaendelea kuitumikia klabu hii kwa muda mrefu,” alisema Xavi.