25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hapatoshi

Pg 1 lowassa*Lissu amjibu JK, asema Lowassa hahusiki na Richmond

Na Waandishi Wetu, Morogoro

MWANASHERIA mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amemkingia kifua mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa akisema hahusiki na sakata la Richmond.

Lissu ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kunukuliwa na gazeti moja akisema kuwa muhusika wa Richmond ni yule anayetembea na Lissu katika kampeni huku akimtaka amtaje kabla Rais Kikwete hajafanya hivyo.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja  vya Shule  ya Msingi  ya Kiwanja  cha  Ndege Manispaa  ya Morogoro jana, Lissu alimtaja kwa jina kigogo wa serikali akisema ndiye muhusika mkuu wa  wa Richmond na si Lowassa.

Kauli hiyo ya Lissu haitofautiani na ile ya Lowassa aliyoitoa alipokuwa akijiunga na Chadema ambapo alisema katika moja ya vikao vya serikali vya kujadili sakata hilo, kiongozi mmoja alisema amepata amri kutoka ngazi za juu kwamba asaini mkataba wa kampuni hiyo.

Lissu alisema ni vema Watanzania kutambua kuwa mmiliki halali wa Richmond ambayo imebadilishwa majina kutoka Dowans hadi Symbion kwa sasa yupo ngazi za juu serikalini.

‘’Huyu mzee wa watu wameshampaka matope vya kutosha na wala hajatoka mbele za watu kulalamika, anatumia busara zaidi.

‘’Tunaishangaa serikali kuendelea kuwadanganya wananchi bila ya huruma kwa kudai kampuni hizo zote zinamilikiwa na Lowassa, kama  kungekuwa na ukweli wowote, kwanini wanaendelea  kulipa hayo madeni  ya mabilioni ya fedha?

“Ni lazima Watanzania watambue kuwa Richmond ilijadiliwa bungeni ikiwa chini ya mwenyekiti wake Dk. Harisson Mwakyembe  ambaye alikuwa kwenye kamati ya Bunge iliyochunguza mkataba wa Kampuni ya Richmond na mwishowe kuja kuibuka kashfa ya mafisadi  ambao walikuwa 11,” alisema na kuongeza.

“Katika mlolongo wa mafisadi waliotajwa namba tisa alitajwa Lowassa wakati akiwa waziri mkuu, lakini hakuhusika moja moja na suala hilo,” alisema.

Lissu alisema katika orodha hiyo namba 10 alitajwa kiongozi mmoja mstaafu na baadae akataja tena jina la kigogo mwingine ambaye alisema huyo ndiye mmiliki wa kampuni hiyo.

Alisema Lowassa ambaye anatembea naye katika kampeni zake hahusiki hata kidogo na suala hilo ila aliwajibika kisiasa ili kuiokoa serikali, kwa kuwa alikuwa msimamizi wa serikali hiyo.

Lissu alisema ili kuondoa mfumo mbovu ni lazima wahakikishe wanaing’oa serikali iliyopo madarakani kwa kipindi cha muda mrefu, kwani hiyo ndio chanzo kikuu cha umaskini.

Lowassa: na wakulima

Kwa upande wake Lowassa, alisema serikali yake itakuwa rafiki kwa wakulima na wafugaji na kuwa atatoa elimu bora bila malipo yoyote.

“Hakutakuwa na mambo ya michango ya ajabu ajabu, tutatoa elimu ya bure lakini iliyo bora,” alisema.

Kuhusu suala la viwanda vya miwa, alisema atahakikisha viwanda vinavyowezekana vitarudishwa mikononi mwa serikali.

Alisema pia kuwa, wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwamo mama lishe na bodaboda, atawahakikisha wanaendelea kuwa rafiki zake.

Sumaye: CCM inahukumiwa kwa uongo wake

Waziri  mkuu  mstaafu, Fredrick Sumaye,  alisema   kwa sasa CCM   inahukumiwa  kwa  kusema  uongo  kwa  kipindi cha  miaka 50 tangu  taifa lipate  uhuru.

Alisema katika kipindi hicho, chama hicho kimeshindwa kukidhi mahitaji muhimu ya Watanzania, hivyo wananchi wamechoka  kudanganywa .

Aidha Sumaye  alidai  Watanzania  bado  wamekuwa  wakiishi  katika mazingira  magumu  na  yenye  shida  pamoja  na CCM  kuja  na  sera  yake  ya  uongo  ya maisha  bora  kwa kila Mtanzania .

“Ni wazi  hakuna  ubishi  kama  Watanzania  sasa  wamechoshwa  na uongo wa CCM, ndio  maana   wametuunga  mkono  kwa  asilimia 100  katika mikutano  yote  ya  Ukawa  pasipo  kuletwa  na magari  kama  ilivyo  katika mikutano  yao”alisema  Sumaye .

Alisema uongo  wa CCM unajionesha  wazi wazi  kwenye  sekta  ya  kilimo, afya , miundombinu, elimu  na  kudai   kuwa  hayo  ni maeneo ambayo  yanawatesa  kwa  kiasi  kikubwa na kuyaona maisha  kuwa  magumu.

Alisema  kuwa  dalili  za  Watanzania  kuunga mkono  ukawa  ni  dalili  tosha  kuonesha  wanahitaji mabadiliko  ndani  ya   taifa , pasipo  kushawishika  na pesa .

“Hapa  mmekuja  kwa  upendo  wenu na taifa lenu hamjaletwa  kwa  magari  kama  ilivyo  katika  mikutano  yao (CCM),” aliongeza  Sumaye .

Naye Mjumbe  wa Kamati  ya Utendaji  Kanda  ya  Kati wa Chadema, Mathew Likwina  akizungumza na  wanachama  wa  chama  hicho alisema  kuwa  lengo  la UKAWA   ni  kufanya  mabadiliko   ya  kimfumo.

Alisema  kuwa  kuondoa  mfumo sio  kubadilisha  kiongozi  mmoja  wa ccm  , bali  ni kuondoa  uongozi  wote  wa  CCM usio  na mfumo mzuri  katika  kuleta maendeleo  ya  taifa  na watu  wake .

Aidha   alidai  kuwa  kama  Watanzania  wataiondoa CCM  taifa  linauhakika  mkubwa   wa  kuwa na mfumo mzuri Wenye  kujali   maslahi  ya wananchi badala  ya  sasa  CCM imekuwa na mifumo  ya  kujali  watu wachache  na  familia  zao .

Habari hii imeandaliwa na Lilian Justice, Ashura Kazinja na Ramadhan Libenanga, Morogoro

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles