23 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Magufuli awavutia pumzi wabadhirifu

Pg 1 magufuli*Awataka wezi wa fedha za wakulima waanze kutubu

Na Bakari Kimwanga, Sikonge

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amewaonya watu wanaofanya uwakala wa kuwaibia wakulima wa tumbaku na kuwataka waanze kutubu kabla hajaingia Ikulu.

Amesema watu hao, wamekuwa wakifanyakazi ya kujinufaisha wao, huku wakulima wa zao hilo wakibaki masikini wa kutupwa.

Dk. Magufuli, alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana  katika mikutano ya kampeni aliyoifanya katika wilaya za Sikonge, Kaliua na Urambo mkoani Tabora.

Alisema ni bora kuanzia sasa, wezi wa fedha za wakulima wakaanza kutubu, badala ya kusubiri mshikemshike hapo baadae.

“Ninajua adha wanayopata wakulima wa zao la tumbaku, natamka hawa wezi siku zao zinahesabika. Narudia kusema ole wao wanao wanyonya kwa kuwaibia wakulima wa tumbaku, najua yote yanayoendelea, kuna watu kazi yao ni kuwaumiza wakulima.

“… Wamekuwa wakinunua tumbaku kwa bei tofauti na bei ya soko la dunia, Serikali ya Magufuli ni tofauti kabisa kama tumbaku ni ya Orange (chungwa), ulipwe kwa uhalisia na kama ni ya limao, ulipwe haki yako kwa mujibu wa bei ya soko,” alisema.

Alisema anajua namna vyama vya ushirika, hasa vile vya msingi vinavyoiba fedha za wakulima, huku viongozi wa vyama hivyo wakiendesha maisha yao vizuri.

“Hata waziri wa kilimo, nitakayemteua kazi yake ya kwanza ni kuhakikisha anasimamia haki zenu. Haiwezekani Appex (chama kilele), kinanufaika kwa makato ya fedha za wakulima…nasema hili kwangu hapana,” alisema.

NKUMBA

Kwa upande wake Mbunge wa Sikonge aliyemaliza muda wake, Said Nkumba jana alijisalimisha kwa Dk. Magufuli na kusema hajajiunga na Chama cha ACT-Wazalendo kama inavyodaiwa na wabaya wake kisiasa.

Nkumba alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi vitatu mfululizo, lakini mwaka huu alikwaa kisiki, baada ya kuangushwa katika kura za maoni ndani ya CCM.

Kujitokeza huko kwa Nkumba, kulisababisha mjumbe wa kamati ya kampeni, Abdallah Bulembo kurusha kombora dhidi ya mwanasiasa kuwa kigeugeu na mhama vyama vya siasa kwa sababu ya kukosa ubunge.

“Leo (jana), tupo hapa Sikonge, kabla sijamleta mgombea urais, niseme kidogo kuhusu taarifa za mdogo wangu, Said Nkumba ambaye baada ya kura za maoni za ubunge alijiunga na Chadema, amekaa siku kadhaa na kuamua kurudi tena CCM.

“Sasa kuna taarifa amejiunga na ACT-Wazalendo, sitaki kuamini kama amekwenda rasmi au laa… jamani ndani ya CCM hakuna mwenye hatimiliki ya ubunge kila mwanachama ana haki ya kugombea, huenda kuna ukweli maana hapa hayupo, ajue CCM itashinda tu na maisha yataendelea,” alisema Bulembo.

Baada ya kutoa maelezo hayo, alimkaribisha Dk. Magufuli jukwaani ambaye alisema anashangazwa na hatua ya Nkumba kuhamahama na kumtaka awe mwanasiasa mvumilivu.

“Nina mdogo wangu, nasikia amekimbia jamani dunia ndivyo ilivyo, Sikonge ina historia yake, maana wamepita wabunge wengi iko vilevile inazidiwa na Chato ya juzi.

“Ninataka kuwaambia uvumilivu ni jambo muhimu  Makalla (Amos), Naibu Waziri wa Maji aligombea pale Mvomero kura hazikutosha  kavumilia jana (juzi) Rais Jakaya Kikwete, amemteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, unapokuwa rais kazi zipo nyingi,” alisema Dk. Magufuli.

Akiwa anaendelea kuhutubia, ghafla  Nkumba alijitokeza katika mkutano huo huku wananchi wakilipuka kwa shangwe.

Dk. Magufuli, alilazimika kumwita jukwaani na kumkabidhi kipaza sauti, huku akimtaka kueleza ukweli kuhusu tukio la kuhama kwake.

Nkumba alitii agizo hilo na kusema hajahma CCM tangu aliporejea Agosti 23, mwaka huu Jangwani jijini Dar es Salaam.

“Mimi siitwi na mwenzangu, ndiyo maana maneno hayaishi, niliitwa na viongozi wa kitaifa na tulishayamaliza. Kwa moyo mkunjufu ninapenda kumuombea kura mdogo wangu John Joseph, madiwani na  rais mtarajiwa Dk. Magufuli mchagueni Oktoba 25 mwaka huu kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Nkumba.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles