Bethsheba Wambura
Serikali ina mpango wa kuunda taasisi ya kushughulikia suala la mradi wa maji vijijini itakayokuwa  chini ya mfuko maalum lengo likiwa kila kijiji kuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama.
Hayo yamesemwa  leo Jumamosi Novemba 3 na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizindua tamasha la mvinyo uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa jijini Dodoma ambapo amesema katika kuhakikisha dhana ya Tanzania ya viwanda lazima kuwepo na maji ya kutosha yatakayotumika majumbani na viwandani.
“Hakuna kiwanda bila maji, miundombinu na mawasiliano ndiyo sababu tunataka kuhakikisha yanapatikana ya kutosha ili kukuza uzalishaji viwandani na kukuza uchumi wetu, “ amesema.
katika hatua nyingine, Makamu wa Rais pia ameziagiza halmashauri za jiji la Dodoma zichukue asilimia ya 10 ya mapato fedha ya ndani  ili kununua viwanda vidogo vya kukamulia zabibu ili wakulima wa zao hilo kupata sehemu maalumu ya kuuzia mazao yao kuepusha kukaa muda mrefu mashambani.
“Dodoma ina jumla ya viwanda 2341 na kati ya hivyo 2308 ni vidogo, 25 vya kati na vinane vikubwa lakini  viwanda vinavyosindika zabibu ni saba pekee, Kwa viwanda vya kati na vikubwa  navyo vina nafasi ya kuchangia katika zao hili na kuongeza mfuko wa viwanda vidogo vidogo
“Tukiweza kutumia fursa zingine za zao la zabibu tutaondoa tatizo la zabibu kuozea shambani, wale waliopewa dhamana ya kufanya tafiti katika kituo cha Mmakutupora waje na teknolojia ya kisasa ya kuongeza thamani katika zao la hili
Aidha serikali imetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji ili kuweka urahisi wa kupatikana ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa shughuli za kiuchumi hasa kilimo na kusaidia wakulima kuanzisha viwanda vidogo vya usindikaji na kuongeza thamani katika mazao yao.