NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
Muiguizaji wa filamu ‘Bongo Movie’ ambae pia aliwahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kuchapisha video ya ngono kupitia mtandaoni wake wa Instagram.
Wema amesomewa mashtaka yake leo Novemba Mosi na wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde.
Mwanaamina anadai mshtakiwa amefanya kosa la kusambaza picha hizo Oktoba 15 mwaka huu katika sehemu tofauti tofauti Dar es Salaam.
Hata hivyo mshtakiwa huyo amekanà mashtaka huku upande wa mashtaka ukidai upelelezi wake haujakamilika hivyo kesi imehairishwa na itatajwa Novemba20 mwaka huu.
Akitoa masharti ya dhamana Hakimu Kasonde amemtaka Wema Sepetu kutoweka video zinazohusiana na ngono wala maneno yoyote yenye mwelekeo huo katika mtandaoni wake wa kijamii wa Instagram.
Pia Wema ametakiwa kuwa na mdhamini mmoja wa kusaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10.
Kabla ya kupewa dhamana hiyo wakili Kombakono aliiomba mahakama kumpatia masharti magumu ya dhamana ili iwe fundisho kwa wengine kwa sababu anawafuasi wengi wanaomuangalia wakiwemo watoto.
Wakili Ruben Simwanza anayemtetea Wema ameomba mteja wake apewe dhamana ya masharti nafuu kwa kuwa ni haki yake.
Mahakama imekubali kumpa dhamana kwa masharti yaliyotajwa.