MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (Chadema), jana ameongoza mamia ya wananchi wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga, wakati wa mazishi ya aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo, marehemu Mohomed Mtoi.
Katika mazishi hayo, Mbowe aliiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ihairishe uchaguzi wa jimbo la Lushoto ili waweze kuanza mchakato wa kutafuta mgombea mwingine wa kuziba nafasi iliyoachwa na marehemu Mtoi ambaye alifariki kwa ajali ya gari juzi.
Alisema uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu katika jimbo hilo hauwezi kufanyika hadi utaratibu wa kupata mgombea mwingine utakapokamilika ukihusisha vyama vyote vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Marehemu Mtoi alizikwa katika Kijiji cha Mkuzi.
Mazishi hayo, yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho, wakiwamo wabunge waliomaliza muda wao ambao ni Joseph Selasini (Rombo), John Mnyika (Ubungo), Halima Mdee (Kawe), Makamu Mwenyekiti, Profesa Mwesiga Baregu, Kaimu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Hassan Hassanali mgombea ubunge Jimbo la Dodoma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, Mnyika alisema kifo hicho ni pengo kubwa kwao na kuwataka wenzao wa CUF kuwafuta machozi kwa kumuunga mkono mgombea wao ambaye watamsimamisha baadae.
“Niseme tumepoteza jembe, nawaomba CUF watufute machozi katika hili kwa kumuunga mkoano mgombea atakayeteuliwa,” alisema.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CUF, Gogola Shechonge akizungumza kuhusu
kauli ya Mnyika kutaka waachiwe jimbo hilo, alisema wamewekeana utaratibu juu ya kuachiana majimbo.