28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Watuhumiwa ujambazi 26 mbaroni Dar

kovaASIFIWE GEORGE NA LUGOLA CHITAGE (TUDARCO), DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikila watu 26 wanaodaiwa kuwa majambazi wanaojihusisha na vitendo mbalimbali vikiwamo vya kuvamia vituo vya polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Suleimani Kova, alisema watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni maalumu iliyoanza Agosti, mwaka huu.

Alisema watuhumiwa hao, walikamatwa na silaha mbili ambazo ziliibwa katika matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi.

Kamanda Kova alisema silaha hizo ni bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) yenye namba za usajili TZPL 26686 iliyoporwa katika Kituo cha Polisi Kimanzichana Juni 26, mwaka jana na nyingine yenye namba TZPL 26706 iliyoporwa Kituo cha Polisi Ikwiriri Januari 21, mwaka huu.

Alisema pia zilipatikana risasi 23 za SMG na magazine mbili katika Kijiji cha Mamdimkongo wilayani Mkuranga.

“Tangu vituo vya polisi vianze kuvamiwa, silaha 27 zimepatikana na majambazi 64 wamekamatwa na kukiri kuhusika na matukio hayo,” alisema Kova.

Alisema katika hali ya kushangaza, jana saa nne asubuhi, mtuhumiwa Ally Uratule (60) mkazi wa Ukonga, Dar es Salaam, alionekana kutaka kutoroka alipokuwa akihojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central).

“Mtuhumiwa alidai anasumbuliwa na tumbo, hivyo kuomba kupelekwa chooni, lakini baada ya kuruhusiwa alionekana kama anataka kujiua au kutoroka, ghafla alijirusha kutoka ghorofa ya tatu hadi chini na kuvunjika mkono,” alisema Kova.

Alisema baada ya kuanguka chini hali haikuwa nzuri, walilazimika kumkimbiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu.

Katika tukio jingine, polisi wanawashikilia watuhumiwa 14 kwa makosa ya ujambazi wa kutumia silaha na uvamizi wa hoteli za jijini Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Kova alisema Agosti 28, mwaka huu maeneo ya Kigogo Luhanga alikamatwa mtuhumiwa Yassin Salehe akiwa na bastola aina ya Revolver yenye namba za usajili 58498 aliyokuwa nayo ndani ya gari lake Toyota Alteza lenye namba za usajili T 936 CHA ambayo hutumika katika matukio ya ujambazi.

“Baada ya kumhoji, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na matukio ya uhalifu akiwa na wenzake ambao ni Elisha Simon mkazi wa Tabata na Emmanuel Denis, aliyekamatwa Sinza akiwa na gari lenye namba za usajili T 616 BJM Toyota Mark ll.

“Katika mwendelezo wa tukio hilo, Septemba 4 mwaka huu alikamatwa mtuhumiwa Elineema Paulo mkazi wa Kimara Makoka, alipopekuliwa alikutwa na bastola aina ya Bereta iliyofutwa namba, ikiwa na risasi saba ndani ya magazine na alikiri kuhusika katika matukio ya uporaji wa kutumia silaha, ikiwa ni pamoja na kuvamia Hoteli ya BNB iliyopo Mwenge, Rombo Green View iliyopo Shekilango, NIC Hotel iliyopo Ubungo Terminal pamoja na hoteli nyinginezo,” alisema Kova.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles