Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MWANASHERIA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mabere Marando, amepelekwa nchini India na familia yake kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano Msaidizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), John Steven, alisema Marando aliondoka juzi na baadhi ya ndugu zake.
“Wameondoka Jumapili kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu zaidi, wenyewe walisisitiza tusitaje ugonjwa unaomsumbua ndugu yao, na kwamba ataeleza mwenyewe (Marando) pindi atakapopona,” alisema.
Marando ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema, alifikishwa hospitalini hapo usiku wa Septemba 7, mwaka huu, baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani kwake.
Alilazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete karibu wiki nzima kwa ajili ya matibabu.