WAKATI dunia ikisherehekea mafanikio  katika nyanja za sayansi na teknolojia, waandishi wa habari wanasherehekea   makaburi ya kuwazika.
Oktoba 9 mwaka huu, dunia imepatwa na mshtuko baada ya kupata taarifa kuwa mwandishi wa habari raia wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi ametoweka ghafla katika ubalozi mdogo wa taifa hilo katika jiji la Instabul nchini Uturuki.
Kupotea katika mazingira ya kutatanisha nguli huyu wa habari aliyewahi kuwa mhariri mkuu wa gazeti la serikali nchini Saudi  Arabia, kunatokana na mazoea yake  ya kuendelea kuukosoa utawala wa kifalme wa nchi hiyo.
Khashoggi ambaye kabla ya kupotea alikuwa akiliandikia gazeti la Washington Post la nchini Marekani, inasemekana aliteswa kikatili na baadaye kuuawa na maafisa usalama kutoka Saudi Arabia katika ubalozi huo ambako alikuwa amekwenda kwa ajili ya shughuli binafsi ikiwemo kuomba kibali cha kuoa.
Ni dhahiri kuwa hata kama utawala wa kifalme wa Saudi Arabia umekanusha kuhusika na mauaji hayo, lakini mazingira yanayokwenda sambamba na muda ambao tukio limefanyika, ni ushahidi tosha kuwa ufalme ndiyo umetenda dhambi hiyo.
Kuuawa kwa Khashoggi ambaye kimsingi alikuwa nembo ya waandishi wa habari shujaa katika kutetea uhuru wa kujieleza, ni mwendelezo wa wanahabari wengi ambao wanaendelea kupoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo watawala  wasiopenda kukosolewa.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2016 iliyotolewa na shirika la elimu sayansi na utamaduni la umoja wa mataifa Unesco, ni kwamba takriban waandishi wa habari 213 waliuawa mwaka 2015, hivyo kuwa mwaka wa pili ambao wanahabari wengi waliuawa ukilinganisha na miaka kumi iliyopita.
Kwa upande wake shirikisho la kimataifa la waandishi wa habari ( International Federation of Journalists) lilitoa ripoti iliyoonyesha kuwa takribani wanahabari 81 walipoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mizozo ya kisiasa.
Ripoti nyingine ya mwaka 2018 ya waandishi wa habari wasio na mipaka yenye kichwa cha habari ‘‘chuki dhidi  ya uandishi wa habari kitisho kwa demokrasia’’  imeelezea kuwa kila bara kuna ongezeko la uhasama dhidi ya vyombo vya habari kunakohamasishwa na viongozi wa kisiasa pamoja na tawala za kiimla zenye kutopendelea demokrasia.
Ripoti hiyo inaendelea kuelezea kuwa mataifa ya China, Urusi, Uturuki na Misri ni miongoni mwa mataifa yasiyofuata  demokrasia na hivyo kuendelea kuwa tishio kwa waandishi wa habari.
Si tu mataifa yasiyo na demokrasia pia ripoti hiyo imekwenda mbali kwa kuonyesha kuwa hata viongozi waliochaguliwa kidemokrasia siku hizi wanavichukulia vyombo vya habari kama si kitu muhimu katika ujenzi wa demokrasia.
Baadhi ya viongozi waliochaguliwa kidemokrasia huku wakiongoza kama watawala wa kiimla ni kutoka katika nchi za Ulaya ya Mashariki mfano Slovakia na Jamhuri ya Cheki ambako waandishi wako hatarini.
Kadhia kwa waandishi wa habari inayagusa pia mataifa ya Afrika kwani na penyewe  wamekuwa wakiteswa, kupotezwa, kufungwa jela na wakati mwingine kuuawa.
Marekani taifa kubwa linalojigamba kutetea uhuru wa kujieleza, nalo limemulikwa na ripoti hiyo kuwa tangu  Donald Trump aingie madarakani, viwango vya uhuru wa habari vimekuwa vikiporomoka ukilinganisha na utawala uliotangulia wa Barack Obama.
Khashoggi  amelazimishwa kutangulia mbele ya haki katika mazingira ya kunyofolewa roho. Je ni zamu ya mwandishi yupi wa habari atamfuata huko aliko katika mazingira yale yale ya kuchinjwa kama mbuzi kutokana na dunia hii kuendelea kujaa watawala wa kifashisti?