25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi wapya 25,000 wapangiwa mikopo

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza majina 25,532 ya wanafunzi wapya watakaopata  mikopo kwa awamu ya kwanza, wenye thamani ya Sh bilioni 88.36.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema   wanafunzi wa kiume ni 16,085 na wa kike ni 9,447.

Alisema bodi hiyo imetangaza orodha hiyo baada ya kupokea orodha ya udahili ya wanafunzi 49,000 kutoka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

“Kwa awamu ya kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2018/19   wanafunzi 25,532 wamefanikiwa kupata mkopo wenye thamni ya Sh bilioni 88.36,” alisema Badru.

Alisema tayari fedha za robo ya kwanza ya mwaka wa masomo imekwisha kutolewa na Hazina Sh bilioni 137.06 kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo 123,285.

“Fedha hizi tutaanza kuzipeleka vyuoni wanakosoma wanafunzi mapema iwezekenavyo  kuwaepusha usumbufu wa kufikiria mikopo badala ya masomo,” alisema Badru.

Alisema katika awamu hiyo bodi hiyo imetoa  Sh milioni 850.35 kwa wanafunzi 69 wanaoendelea na masomo nje ya nchi kwa  makubaliano maalumu na nchi rafiki saba.

Badru alisema  awamu nyingine ya orodha ya mikopo itatolewa baada ya waombaji wengine kupata taarifa zao na ambao watakata rufaa.

“Tutafungua dirisha la rufaa hivi karibuni  kuwapa fursa waliokuwa wamechelewa kupata baadhi ya nyaraka au kukosea kurekebisha taarifa zao,” alisema Badru.

Alisema wataendelea kutoa orodha nyingine kadri bodi hiyo itakavyokamilisha uchambuzi wa orodha za wanafunzi walioomba mikopo na ambao watapata kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja  kuhakikisha fedha zinawafikia walengwa.

Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Dk. Veronica Nyahende, alisema mikopo ya wanafunzi wa mwaka wa pili itatolewa ikiwa wanafunzi hao wamefaulu mitihani yao na matokeo kuwasilishwa HESLB na vyuo husika.

“Mpaka sasa vyuo 10 bado havijawasilisha matokeo ya wanafunzi wao hivyo tunaviomba vifanye hivyo tuweze kutimiza majukumu ya kuwapatia mikopo wanafunzi hawa,” alisema Dk. Veronica.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles