Na Bakari Kimwanga
OKTOBA 25, mwaka huu macho na masikio yatakuwa jijini Lagos nchini Nigeria kwenye mkutano mkubwa wa wajasiriamali ambao unakutanisha watu zaidi ya 5000 kutoka nchi za Afrika chini ya uratibu wa Taasisi ya Tony Elumelu.
Mkutano huo mkubwa unaokutanisha mataifa ya Afrika sasa unakwenda kufungua milango kwa wajasiriamali ambao ndiyo wameshika usukani katika kuimarisha uchumi wa nchi hizo.
Tanzania ni moja ya nchi za Afrika ambazo nayo itakuwa na uwakilishi kwenye mkutano huo, huku ikitajwa ni moja ya nchi ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi.
Tangu mwaka 2017 kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania imefikia asilimia 7 na moja ya chachu ya kasi hiyo inatajwa kuwa ni biashara ndogondogo ambazo kwa kiasi kikubwa zinamilikiwa na wanawake.
Kwa mujibu wa Takwimu za usawa wa kijinsia katika ajira zinaonesha kwamba kufikia mwaka 2014 Watanzania milioni 2.1 walikuwa wameajiriwa katika sekta rasmi, pamoja na serikalini na sekta binafsi, kwa mujibu wa kituo cha taifa cha takwimu nchini humo.
Hata hivyo takwimu rasmi za serikali zinaonesha pia kwamba zaidi ya asilimia 60 ya wanawake walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 24 yaani milioni 13.9 wanajishughulisha na shughuli zisizo rasmi yaani biashara ndogondogo na kilimo.
Hatua hii maana yake ni kwamba ni asilimia 0.75 tu ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi ndio wapo katika sekta rasmi.
Kwa maneno mengine, idadi kubwa ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi nchini Tanzania ni wajasiriamali.
Pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wanawake wenye ujasiri wa kubuni na kuendesha biashara, kasi ya ukuaji wa mitaji yao bado ni finyu.
Chanzo kikuu cha mitaji karibuni duniani kote ni mikopo rasmi ya kibiashara. Hata hivyo, tafiti zinaonesha kuwa wanawake wengi wajasiriamali kutoka nchi zinazoinukia ikiwamo Tanzania hawana mikopo kutoka benki na taasisi rasmi za kifedha.
Utafiti uliochapishwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2014 unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya maombi ya mikopo ilitengwa kwa ajili ya wajasiriamali wanawake na asilimia 90 iliiva kwa ajili ya kutolewa.
Hata hivyo asilimia 18 ya wanawake wajasiriamali ambao waliomba mikopo benki na asilimia 28 waliomba mikopo katika taasisi nyenginezo za kifedha.
Hatua hiyo inakwenda kuwakutanisha zaidi ya 5,000 wanatarajiwa kukutana mjini Lagos nchini Nigeria kujenga mtandao mkubwa wa sekta hiyo barani Afrika.
Taasisi ya Ushauri wa Ujasiriamali inayoongoza Afrika, Tony Elumelu Foundation (TEF), mkutano huo utafanyika Oktoba 25 ikiwa ni sehemu ya Mkutano Mkuu wa Nne wa Maendeleo ya Kibiashara.
Mkusanyiko huo mkubwa wa wajasiriamali wa Afrika utakaounganisha wajasiriamali zaidi ya 5,000, wawekezaji wa kimataifa, viongozi kutoka sekta za umma na binafsi za Afrika na mashirika ya maendeleo, utafanyika katika Hoteli ya Federal Palace iliyopo jijini Lagos nchini Nigeria.
“Tukio hilo ni fursa ya pekee ya kuzalisha mawazo, kuunda mitandao na kuleta watunga sera na sekta binafsi kwa pamoja ili kuibua mijadala na majadiliano,” ilieleza taarifa hiyo.
Ilieleza kwa kuzingatia rekodi ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ya kuziunganisha taasisi kwa kuwakutanisha wanasiasa ana kwa ana na kizazi kipya cha wanaume na wanawake wafanyabiashara barani Afrika, mkutano huo utahudhuriwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyata, Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo na Mwanzilishi wa Taasisi ya TEF, Tony O. Elumelu.
“Mkutano huo pia utajumuishwa na uzinduzi wa mtandao wa kidijitali – TEFConnect, ambalo litakuwa ni jukwaa kubwa duniani kwa ajili ya kuwaunganisha wajasiriamali wa Afrika na kujengea mazingira ya ujasriamali,” ilieleza taarifa hiyo.
Kupitia taarifa hiyo, mwanzilishi wa taasisi hiyo, Elumelu, alieleza kwamba katika kipindi cha miaka minne waliwafikia wajasiriamali 4,460 na mafanikio yake yameshaanza kuonekana sasa.
“Katika kipindi cha miaka minne tumeweza kuwafikia moja kwa moja wajasiriamali 4,460, na tumeanza kuona matokeo yake kama vile uanzishwaji kazi, lakini ni muhimu zaidi kutambua kuwa ustawi wa kiuchumi wa Afrika unafanywa na wajasiriamali wa kike na wa kiume, wadogo na wakubwa kuwa ni injini ya mabadiliko ya bara letu,” alisema.