Wabunge kupiga kura Uhuru kuongezewa muda

0
1345

NA ISIJI DOMINIC

JE, wabunge katika Bunge la Taifa leo watapiga kura kwa kauli moja kubadilisha tarehe ya uchaguzi mkuu kutoka Agosti hadi Desemba? Au tutarajie vurugu zilizoshuhudiwa mwishoni mwa mwezi uliopita wakati wa kupitisha Muswada wa Fedha 2018?

Awali, wabunge walitarajiwa kupiga kura Jumatano iliyopita lakini Waziri wa Usalama wa Ndani, Dk. Fred Matiang’i, alitangaza Oktoba 10 kuwa ni sikukuu ya Moi Day. Sikukuu hiyo iliondolewa miongoni mwa sherehe za kitaifa kufuatia kupitishwa kwa Katiba Mpya Agosti 2010.

Hata hivyo, uamuzi wa mahakama Novemba mwaka jana iliyotolewa na Jaji George Odunga ilirudisha sherehe hizo ikitoa sababu ya kuondolewa kwa sherehe hizo kunakiuka Sheria ya Sikukuu za Kitaifa.

“Kufuatia uamuzi huo, Oktoba 10 itakuwa sikukuu ya kitaifa,” alisema Dkt. Matiang’i katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Jumatatu ya wiki iliyopita japo hakufafanua namna siku hiyo itakavyosherehekewa.

Mahakama ilieleza hadi Bunge itakapofanya mabadiliko ya sheria kwa kuifuta au Waziri wa Usalama wa Ndani akaibadilisha na sherehe nyingine, Wakenya bado wataendelea kusherehekea sikukuu hiyo iliyoasisiwa na Rais Mstaafu Daniel arap Moi.

Leo ni siku nyingine muhimu kwa wabunge kupiga kura Muswada wa Kubadilisha Katiba ya Kenya 2017 (The Constitution of Kenya (Amendment) Bill 2017) iliyowasilishwa na Mbunge wa Kiminini Dk. Chris Wamalwa.

Kuahirishwa upigaji wa kura kwa wiki moja kumewapa fursa wabunge kufanya kampeni kuhakikisha tarehe ya uchaguzi mkuu inabadilishwa kutoka Jumanne ya pili Agosti hadi Jumatatu ya tatu Desemba na hii itamaanisha Rais Uhuru Kenyatta kuongezwa muda wa kuendelea kukaa ofisini.

Sio tu Rais Uhuru lakini pia wabunge, magavana, maseneta, wawakilishi wa wanawake na wawakilishi wa mabaraza ya kaunti (MCA) kujiongezea muda wa kukaa ofisini kwa miezi minne zaidi.

Dk. Wamalwa alinukuliwa akisema takribani wabunge 250 wameonesha nia ya kuunga mkono muswada huo itakapokuja hatua ya kupigiwa kura. Ili muswada huo kupita itahitaji kuungwa mkono na thuluthi mbili sawa na wabunge 233 kati ya 349.

“Sina wasiwasi muswada huu utapita kwa sababu ninaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge,” alisema Dk. Wamalwa ambaye alikuwa miongoni mwa wabunge kutoka Mkoa wa Magharibi waliomtembelea Rais Uhuru wiki iliyopita Ikulu jijini Nairobi.

Hoja iliyowasilishwa na Dk. Wamalwa kutaka tarehe kubadilishwa ni kwamba uchaguzi mkuu inapaswa kufanyika tarehe ambayo haimbughudhi Mkenya yeyote akisisitiza uchaguzi kufanyika Agosti inaweza ikaathiri mitihani ya kitaifa.

Mfano mzuri ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana uliofanyika Agosti ambapo matokeo yake yalibadilishwa na Mahakama ya Juu na kuamuru urudiwe ndani ya siku 60 ambapo yaliingiliana na mitihani ya kitaifa ambayo hufanyika kuanzia mwishoni mwa Oktoba.

Kizingiti ambacho kinaweza kukumbana nalo muswada huo wa kubadilisha tarehe ya uchaguzi itakayomuongezea muda wa kukaa madarakani Rais ni kura ya maoni. Muswada huo utapelekwa Bunge la Seneti endapo wabunge wataupitisha. Na Seneti nao wakiupitisha, maspika wa mabunge yote mawili kwa pamoja wataiwasilisha kwa Rais Uhuru ili aweke saini.

Hata hivyo kabla ya kusaini, Rais atatafuta ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama muswada huu utahitaji kura ya maoni. Kwa kawaida si jukumu la maspika hao wawili kuamua kufanyika kwa kura ya maoni.

Mswada huu wa kubadili tarehe ya uchaguzi ambao leo wabunge wataupigia kura mara mbili uliwahi kuwasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Ugenya, David Ochieng’, mwaka 2014 na 2015 lakini ulikwama kutokana na idadi ndogo ya wabunge waliyohudhuria kikao hicho.

Kuna kila dalili wabunge wataupitisha muswada uliowasilishwa na Dk. Wamalwa kwa sababu itamaanisha kuendelea kutumikia watu wa eneo lao la ubunge kwa miezi minne zaidi na hivyo kuendelea kupokea mshahara na posho itokanayo na vikao vya bunge.

Lakini Rais Kenyatta bado anayo mamlaka ya mwisho kama muswada huo licha ya kupitishwa na idadi ya wabunge wengi kama itapigiwa kura ya maoni. Aidha kupitishwa kwa muswada wa kubadilisha tarehe ya uchaguzi kunaweza kuamsha vuguvugu la kura ya maoni yenye nia ya kupunguza gharama ya maisha hususani baada ya ushuru wa bidhaa itokanayo na petrol kuongezwa kwa asilimia nane.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here