PARIS, UFARANSA
KOCHA wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps, ameshtushwa na uamuzi wa kustaafu kucheza michezo ya kimataifa uliotolewa na beki wake, Laurent Koscielny.
Koscielny, ambaye ni beki katika timu ya Arsenal, inayocheza Ligi Kuu England, alitoa uamuzi huo hivi karibuni, wakati akiendelea kuuguza jeraha lake la misuli ya paja ambalo pia lilimfanya kukosa michezo ya Kombe la Dunia.
Hata hivyo, beki huyo alifanya uamuzi huo huku akilalamika kwamba hana mawasiliano mazuri na kocha wa timu ya taifa, Deschamps.
Akizungumzia uamuzi huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari juzi, Deschamps alisema: “Ninaelewa hali halisi wakati akizungumzia kuhusu uhusiano, lakini nilishtuka kwa uamuzi wake kama ambavyo wafanyakazi wengine wameshtushwa.”
“Wafanyakazi walionyesha namna ambavyo wameshtushwa. Nilimwita baada ya kupata jeraha, hata alipoamua kufanyiwa upasuaji nilimwita pia kujumuika nasi wakati wa kujiandaa na michuano ya Kombe la Dunia.
“Septemba mwaka huu ilikuwa siku yake ya kuzaliwa, nilifanikiwa kuzungumza naye kufahamu hali yake kiafya.”
Deschamps alisema kuwa: “Haitabadilika kuwa Koscielny ni mchezaji mkubwa ambaye ana thamani duniani.”