VIWANJA vya Leaders Club kesho vinatarajiwa kuwaka moto wakati wasanii watakapokuwa wakitumbuiza katika uzinduzi wa tamasha jipya la KiliFest 2015, linalodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
Ili tamasha hili la KiliFest liwe na hadhi kubwa, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli, anasema limeandaliwa kwa umakini mkubwa, huku wasanii wakali na wenye majina makubwa nchini wakitarajiwa kulinogesha.
Wasanii wanaotarajiwa kupamba tamasha hilo ni Mapacha Watatu, Kundi la Weusi, Maua, Ruby, Damian Soul, Vanessa Mdee, Ben Pol, Fid Q, Isha Mashauzi na Shettah.
Pamela anasema wasanii wote hao wana nguvu na uwezo wa kuimba live, kitu ambacho Watanzania wanakitaka kutoka kwao hiyo kesho.
“Tunachukua nafasi hii kuwaweka kwenye hatua nyingine kimuziki na pia kuwapa nafasi ya kupata ofa nyingi zaidi ndani na nje ya nchi,” anasema Pamela.
Kwa upande wa wasanii watakaoshiriki tamasha hilo, wamewataka mashabiki wao na wapenda burudani kwa ujumla wajitokeze kwa wingi kwa kuwa wamewaandalia vitu tofauti na ‘surprise’ nyingi kwa ajili yao.
George Sixtus Mdemu (G –Nako/G-Warawara), na Nickson Saimon (Niki wa pili) kutoka kundi la Weusi, wameahidi kutowaangusha mashabiki wao, huku wakipongeza bia hiyo kubuni tamasha hilo la aina yake.
Wanadada waliojizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania kwa nyimbo zao nzuri na shoo nzuri zinazofanywa nao, wakishirikiana na madansa wao, Vanessa Mdee (Vee Money) na Ruby, wanatarajiwa kung’ara na sauti zao tamu zifikapo masikioni kwa mashabiki wao.
Wasanii wengine wanaojinadi kufanya vizuri katika tamasha hilo ni mkali wa hip hop, Fid Q, aliyeanza muziki miaka ya 90 na kujivunia nyimbo zake nyingi zenye mafunzo, ukiwemo wa ‘Huyu na Yule’, uliorekodiwa mwaka wa 2000.
Mkali wa Bongo Flava, Shettah, anayetamba na wimbo wa ‘Kerewa’, mkali wa muziki laini wenye vionjo vya mapenzi, Ben Pol, anayetamba na wimbo wake wa ‘Sophia’ na mkali wa sauti, Damian Soul wanatarajiwa kukonga nyoyo za idadi kubwa ya mashabiki inayotabiriwa kufika kesho katika viwanja hivyo.
Pia tamasha hilo litapambwa na Bendi ya Mapacha Watatu, likiwa na waimbaji wake wakali, Khalid Chokoraa na Jose Mara. Lakini pia muziki wa taarabu haukusahaulika, kwani Isha Mashauzi ambaye ni mtunzi bora wa muziki huo nchini na mkali mwingine anayekuja kwa kasi katika uimbaji, Maua Sama, watakonga nyoyo za mashabiki katika tamasha hilo.
Ili kutoa nafasi kwa wadau wengi wa burudani na wapenda burudani kwa ujumla, Pamela ameweka wazi kwamba tiketi za tamasha hilo ni Sh 10,000 na milango ya Leaders itakuwa wazi kuanzia saa nne asubuhi ambapo shughuli mbalimbali zitaendelea.