25.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Shigella atoa ufafanuzi bajeti kubwa ya elimu

Na Amina Omari-Kilindi

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella, amesema bajeti kubwa inayotengwa na Serikali katika sekta ya elimu, inalenga kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora.

Aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa majengo ya chuo cha ufundi ikiwa ni mradi uliofadhiliwa na Shirika la World Vision uliofanyika katika Tarafa ya Mswaki, Kata ya Mabalanga wilayani Kilindi.

Shigella alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaweka kipaumbele katika sekta ya elimu kwani inatambua bila elimu hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.

Alisema kila mwezi Serikali inatoa Sh bilioni moja kama sehemu ya ruzuku ya kusomesha watoto.

“Nimefurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Shirika la World Vision, naona mnaunga mkono kwa vitendo jitihada zinazofanywa na Serikali ili watoto wa masikini waweze kusoma na kuondokana na umasikini,” alisema Shigella.

Alisema katika kuunga mkono jitihada hizo, atahakikisha mwakani chuo hicho kinapata usajili ili wanafunzi watakaosoma waweze kuwa na vigezo vizuri vitakavyowawezesha kuajiriwa.

“Nitaongea na wenye mamlaka waje wafanye ukaguzi waweze kujiridhisha na hali ya utoaji wa taaluma na miundombinu ili wakamilishe taratibu,” alisema Shigella.

Mkurugenzi wa miradi World Vision Tanzania, Johnson Robinson, alisema shirika hilo lina zaidi ya miradi saba katika Mkoa wa Tanga ambayo wanaifanya kwa kushirikisha jamii.

Alisema sehemu kubwa ya miradi wanayoitekeleza inatokana na kuibuliwa na jamii yenyewe, hivyo aliiomba Serikali kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi ili miradi hiyo iweze kuwa endelevu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles