NA VERONICA ROMWALD – BAGAMOYO
MAGARI ya watu binafsi ndiyo yanaongoza kwa ajali za barabarani ikilinganishwa na yale ya abiria na umma.
Hayo yalielezwa mjini hapa jana na Mwanasheria wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Deus Sokoni, wakati akiwasilisha mada kwenye semina maalumu kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya usalama barabarani.
“Mwaka 2016, katika jumla ya ajali 9,856 zilizokuwa zimetokea, gari binafsi zilikuwa 3,649, mabasi 346, daladala 947, taxi 166, gari za kukodi 120, malori 920, pikipiki 2,544, baiskeli 271, pick-up 884 na mikokoteni ilikuwa tisa,” alisema.
Kamanda Sokoni ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati inayohusu masuala ya usalama barabarani nchini (Bloomberg), alisema madereva wengi huendesha gari bila kujali usalama wao na wale waliowabeba.
“Baadhi tunaona wana dharau, wanakunywa pombe, wanalewa wanaendesha gari bila kujali, hata faini wanaona wanao uwezo wa kulipa.
“Tofauti na dereva wa vyombo vingine kwa mfano daladala au mabasi wanaendesha wakiwa na hofu, kwamba ikiwa atasababisha ajali mzigo wa faini utakuwa ni wa kwake, anaweza kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi, ikiwamo hata kufutiwa leseni,” alisema.