25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Figisu Uchaguzi Mkuu zaanza Z’bar

Na KHAMIS SHARIF -ZANZIBAR

WAKATI Wakala wa Usajili na Matokeo ya Jamii Zanzibar, ukiendelea kusajili wananchi vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, figisu za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 zimeibuka.

Kuibuka kwa hali hiyo kunatokana na madai ya baadhi ya wananchi kuzuiwa kujiandikisha kwa kile kilichoelezwa sababu za kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Unguja, Mbunge wa Malindi, Ali Salehe (CUF) alisema hatua ya wananchi jimboni kwake kuzuiwa kujiandikisha kupata vitambulisho hivyo ni mkakati wa makusudi wenye lengo la kisiasa na usiojali haki za watu.

Alisema mbali na wananchi wa jimbo lake, lakini katika baadhi ya maeneo mengine pia kumekuwa na mkakati wa kuzuiwa watu jambo ambalo halikubaliki na aliitaka Serikali kuwa makini kwa kuingilia kati hali hiyo.

Mbunge huyo alisema licha ya wananchi wengine kupoteza vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, kuhama na wengine ni vijana waliofikisha umri wa miaka 18, lakini bado wamekuwa wakikutana na vikwazo vya kuvikosa hali ya kuwa ni haki yao kwa mujibu wa sheria.

Alisema suala la usajili wa vitambulisho hivyo ni haki ya kila Mzanzibari ambaye ametimiza sheria, vigezo na masharti ya ukaazi, lakini jambo la ajabu ni pale wale wenye sifa wanazuiwa kupata haki yao.

“Sheria haisemi kuwa kama vijana wapya wana siku yao ya kujiandikisha wakati Mzanzibari aliyefikia miaka 18 anayo haki ya kujiandikisha, sasa hawa wakija kujiandikisha wanakumbana na usumbufu mkubwa,” alisema Salehe.

Mmoja wa vijana aliyekumbana na kadhia hiyo kwa kunyimwa usajili wa kitambulisho, Juma Abdallah Khamis alisema kitambulisho ni haki kwa kila Mzanzibari kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini kuna dosari ikiwa vijana waliomaliza shule wananyimwa haki yao.

Khamis alisema kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi ni msingi wa maisha na pindi wao wanaponyimwa ni kusababishiwa usumbufu.

Alisema ikiwa mtu atakosa kitambulisho hicho hupata usumbufu ikiwemo kukosa vigezo vya kuomba vyuo vya elimu ya juu, bima ya afya, kufungua akaunti benki na mahitaji mengine muhimu.

Nao wakazi wa Mpendae na Migombani ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema usajili huo umekuwa ukiendeshwa kisiasa.

“Zoezi ni gumu sana kwa sababu sisi wangine leo siku ya nne tunakuja bila ya mafanikio, tunapigwa jua, wenzetu wengine wanatoa shilingi 5,000 kwa watu na wanapitishwa kwenye milango na watu na wengine wanajikuta wakiliwa pesa zao tu,” alisema mmoja wa wakazi hao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usajili wa Matokeo ya Kijamii Zanzibar, Dk. Hussein Shaaban, kupitia taarifa yake kwa umma, alisema vitambulisho ni haki ya kila raia mwenye sifa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Dk. Shaaban alisema usajili huo unaendeshwa chini ya Sheria Na 3 ya mwaka 2018 ambayo imetoa maamuzi kila mtu mwenye masharti kusajiliwa bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Alisema usajili huo unahusu kuimarisha taarifa za wananchi wote wenye vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZEN ID), wakiwamo waombaji wapya na wanaobadilisha shehia au makazi.

“Ili mtu aweze kupata kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi katika shehia husika ambayo anaishi, anatakiwa kuwa na cheti cha kuzaliwa sambamba na barua kutoka kwa sheha wa shehia husika.

“Kwa wananchi wanaobadilisha maeneo ya kuishi wanapaswa kuwa na vielelezo vya kuthibitisha ukaazi wao kutoka katika shehia zao mpya tu waweze kupata haki yao hiyo,” alisema Dk. Shaaban.

Kwa muda mrefu suala la vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi limekuwa likiibuka na hata kudaiwa kuingiliwa na maamuzi ya wanasiasa kwa malengo wanayoyajua wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles