NA MOHAMED MHARIZO, DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF), limepanga kuzuia timu zake kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar, kutokana na Chama cha Mpira wa Miguu visiwani humo (ZFA), kukabiliwa na kesi mahakamani.
Rais wa wa TFF, Jamal Malinzi, amesema Dar es Salaam jana katika mahojiano maalumu na MTANZANIA kuwa wana kila sababu ya kuzizuia timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kwenda Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi.
Alisema ZFA ina usajili wake katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), hivyo ni vigumu wao kuingilia mgogoro wao, zaidi ya kuwashauri wamalize tofauti zao na kuondoa kesi mahakamani kwa kuwa ni kinyume cha taratibu za mchezo huo, kufungua kesi katika mahakama za kiraia.
“Mambo haya yanapaswa yaondolewe mahakamani na ZFA wafanye maridhiano ili mpira uendelee kuchezwa Zanzibar, sasa kwa hali hii hata TFF haiwezi kuruhusu timu zake kwenda kucheza Kombe la Mapinduzi, wakati kuna masuala ya mpira yamepelekwa mahakamani.
“Hata CAF wakisikia TFF timu zetu zinacheza itaonekana na sisi tunashirikiana nao katika masuala haya, jambo ambalo linaweza kutuweka katika wakati mgumu,” alisema Malinzi.
TFF inaweza kufikia hatua hiyo ya kutishia kuondoa timu zake kushiriki Kombe la Mapinduzi, linalofanyika kila mwezi Januari visiwani kutokana na ZFA kuwa na kesi mbili mahakamani.
Kesi ya kwanza ni ile inayowakabili viongozi wa juu wa ZFA, katika Mahakama Kuu ya Vuga, iliyofunguliwa na Makamu wa Rais wa ZFA Unguja, Haji Ameir Haji. Haji alifungua kesi nambari 62/2014 dhidi ya Rais wa ZFA, Ravia Idarous Faina, Makamu wa Rais wa ZFA, Pemba Ali Mohammed Ali na Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Haji Salum, akidai kukiukwa kwa utaratibu wa kuifanyia marekebisho katiba ya chama hicho, kukiukwa kwa taratibu za matumizi ya fedha na kuwepo kwa ubaguzi katika uongozi wa chama hicho.
Kesi nyingine inayoikabili ZFA ni ile iliyofunguliwa na timu ya Chuoni katika Mahakama ya Mkoa wa Mjini, iliyopo Mwanakwerekwe, ikipinga kushushwa Daraja la Kwanza kutoka Ligi Kuu. Kutokana na kesi hiyo, iliyofunguliwa Agosti 20 mwaka huu, timu ya Chuoni imetaka Ligi Kuu iliyopangwa kuanza Septemba 15, kusimamishwa hadi suala lao litakapopatiwa ufumbuzi.