32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU: NAKWENDA MAHAKAMANI


Na AGATHA CHARLES

MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema atalifikisha Mahakama Kuu suala la gharama za matibabu yake ili iweze kutoa tafsiri sahihi baada ya Bunge kushindwa kumlipia.

Lissu aliyasema hayo kupitia andiko lake lililoanza kusambaa jana akiwa anatimiza mwaka mmoja tangu alipopigwa risasi Septemba 7, mwaka jana eneo la nyumbani kwake jijini Dodoma.

Katika andiko  lake hilo ambalo pia  ameelezea tukio zima la kujeruhiwa kwake,  mwenendo wa matibabu katika kipindi chote cha mwaka mmoja na kile alichodai kiini cha kuumizwa kwake, kuhusu suala la matibabu ambalo amelifafanua kwa kina  Lissu ametoa sababu za kimazingira na kisheria  ambazo ndio msingi wa yeye kuamua kulifikisha suala hilo mahakamani.

“Kwa upande wetu, njia pekee iliyobaki sasa ni kulipeleka suala hili mahakamani ili Mahakama Kuu itoe tafsiri sahihi ya jambo hili. Maandalizi ya kwenda mahakamani yanaendelea,” alisema Lissu.

Akirejea mvutano kuhusu Bunge kukataa kulipia gharama za matibabu yake,  Lissu aliuelezea kama ‘mgogoro wa kutengenezwa’ ambao katikati yake yumo Spika wa Bunge, Job Ndugai na Katibu wa chombo hicho, Steven Kagaigai ambao wamekuwa wakidai alikiuka taratibu za matibabu ya wabunge kwa kupelekwa Nairobi badala ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwanza.

Katika hilo Lissu alisema utaratibu huo hautambuliki kisheria jambo linaloonekana Spika Ndugai amekubali kuingiliwa na kupokwa madaraka ya Bunge kuendesha shughuli zake kama mhimili huru wa dola.

Akifafanua kuhusu sheria hiyo inayohusika na matibabu ya Wabunge alisema ni Sheria ya Uendeshaji wa Bunge ya mwaka  2008 ambayo inaeleza kwa kifupi kwamba kila mbunge atakuwa na haki ya kutibiwa ndani au nje ya Tanzania kwa gharama ya Bunge.

“Utaratibu wa kupata kibali cha Muhimbili, au cha Katibu Mkuu Afya, au cha Rais haupo kwenye Sheria hiyo.

Lissu alisema kama utaratibu huo ungekuwepo kisheria, bado ulikuwa haukidhi na usingeweza kukidhi mahitaji ya dharura iliyotokana na kushambuliwa kwake.

“Kwa majeraha nikiyokuwa nayo na kwa hali ya kiusalama iliyokuwepo, hakukuwa na uhakika kwamba nikipelekwa Muhimbili nitakuwa salama dhidi ya watu walionishambulia.

 

“Na hakukuwa na muda mrefu wa kusubiri hali itulie ndio taratibu zinazosemwa zifuatwe. Ilibidi uamuzi ufanywe haraka ili nikapatiwe matibabu katika hali ya dharura ya kiafya na kiusalama iliyokuwepo”, linasomeka andiko lake hilo.

Alisema uamuzi na taratibu zote za kumpeleka hospitali ya Nairobi haukufanywa na uongozi wa juu wa Chadema peke yao bali ulihusisha viongozi wengine wa Bunge na Serikali  na hivyo kuhoji utaratibu aliokiukwa.

Alisema baada ya kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kilifanyika kikao kilichowahusisha viongozi wa Chadema, Bunge na Serikali kuhusu hatua za kuchukua.

Alisema upande wa Chadema uliongozwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, na  Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wabunge kadhaa na upande wa Bunge uliongozwa na  Spika Ndugai, Naibu Spika Tulia Akson na Katibu wa Bunge wakati huo, Dk. Thomas Kashililah wakati upande wa serikali alikuwepo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu wake Dk. Ulisubisya Mpoki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

“Kikao hicho ndicho kilichoamua nipelekwe Nairobi. Ndio maana katika msafara ulionipeleka Nairobi Hospitali, alikuwepo pia Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma”, alieleza Lissu.

 

Kutokana na hayo alisema ndio maana ndege iliyompeleka Nairobi iliruhusiwa kuruka Uwanja wa Ndege wa Dodoma saa sita usiku.

“Ningekuwa nimepelekwa Nairobi kwa utaratibu binafsi, kama inavyodaiwa sasa, nisingesindikizwa na Mganga Mkuu wa Mkoa na wala Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) isingeruhusu ndege kuondoka Dodoma saa sita usiku.

“Na wala maafisa wa uhamiaji wasingegonga muhuri passport zetu na kuturuhusu kutoka nje ya nchi”, alieleza.

Alisema baada ya kuwa ameshapokelewa hospitali ya Nairobi na maisha yake  kuokolewa, Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kashililah walikutana na ndugu zake kwenye Ofisi ya Bunge Dar es salaam  na kuwashauri waandike barua rasmi ya maombi ili Bunge liweze kutoa fedha za matibabu yangu.

Lissu alieleza kuwa Waziri wa Afya, Ummy naye alishauri hivyo hivyo, tena hadharani kwenye mkutano na wandishi habari.

Alieleza kuwa Ummy alisisitiza jambo hilo kwa kutoa mfano wa Spika wa zamani wa Bunge, marehemu Samuel Sitta, ambaye inasemekana aliomba msaada wa kutibiwa na Bunge wakati hakuwa Mbunge tena, na tayari alikuwa hospitalini London, Uingereza.

“Barua zikaandikwa na ndugu zangu kama walivyoelekezwa na uongozi wa Bunge. Lakini mara Katibu wa Bunge Kashililah akaondolewa madarakani na Rais Magufuli, na Steven Kagaigai akateuliwa kushika nafasi hiyo”, alieleza.

Alieleza kuwa inavyoonekana Kagaigai alikwenda na maelekezo ya yeye kutopewa fedha yoyote ya matibabu na Bunge.

KIGAIGAI AJIBU

MTANZANIA Jumamosi jana  liliwasiliana na Kagaigai kuhusiana na madai hayo ya Lissu kwamba yuko pale kwa maelekezo kuwa asitoe fedha za matibabu ambapo alisema;

“Kama ana ‘just course’ mimi nitasema nini kwenye hilo, ungekuwa wewe ungemwambia acha au nenda?, huwezi kumwambia acha au nenda hiyo ni juu yake!

“Hajawahi kuandika barua kuomba fedha, labda kama aliandika wakati huo labda, ila mimi sijaiona hiyo barua lakini barua kuhusiana na matibabu yake alishawahi kuandika na hiyo imeshajibiwa mara kadhaa na Spika wa Bunge na ninyi mna taarifa  na alishaeleza mara kadhaa ndani ya Bunge.

“Kwa hiyo kunihusisha mimi na hilo nadhani ni kunikosea kabisa sioni kama ni sawa,” alisema

 

AHOJI UCHUNGUZI

Katika andiko lake hilo Lissu pia ameelezea sababu za kushambuliwa kwake akisema walitaka afe kwa sababu ya msimamo wake kisiasa na si shughuli zake za uwakili ambazo amezifanya kwa muda mrefu pasipo kusumbuliwa.

Lissu pia alihoji na kushangazwa na uchunguzi kuchukua muda mrefu hasa ikizingatiwa kuwa katika eneo ambalo tukio hilo lilitekelezwa kulikuwa na kamera za usalama (CCTV).

 

HEMED ASIMULIA ALIVYOMPOKEA

LISSU NAIROBI

Wakati Lissu akieleza hayo kwa upande wake Mkuu wa Idara ya uenezi wa Chadema, Hemed Ally naye aliandika akielezea namna tukio hilo lilivyomgusa na zaidi alivyoshiriki kumpokea Lissu Nairobi na kisha kumkimbiza hospitali.

Alisema yeye ndiye aliyefanya mipango ya kumpokea Lissu kwa msaada wa marafiki zao wa muungano wa Jubilee akiwa Nairobi baada ya kupigiwa simu na Mbowe.

Akielezea jinsi Lissu alivyoumia alisema mwili na nyama zake zilichambuliwa na risasi zaidi ya 38 na kwamba damu na vipande vya nyama ndio uliokuwa muonekano wake.

Hemed katika andiko lake hilo alisema baada ya kumfikisha hospitali ya Nairobi ambayo alielezwa kuwa ni nzuri, kwa jinsi Lissu alivyokuwa ameumia hata walipoambiwa na daktari waende kupumzika haikuwa rahisi kwa yeyote kati yao aliyeonja usingizi.

Hemed pia alisimulia kazi nzito aliyopewa na Mbowe ya kukaa na Lissu hospitalini hapo.

Akihitimisha andiko lake, Hemed mbali na kulaani tukio hilo na zaidi kumwombea kwa Mungu Lissu apone haraka  alisema anaamini kesho yao ya vita hiyo ni neema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles