23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MGAMBO WA MAKONDA KORTINI


NA PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

Askari mgambo wawili, Kelvin Sawala (25), Goodluck Tarimo (30) na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bunju, Ibrahim Mabewa (39), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kosa la kumsababishia majeraha kwa kutumia rungu mkazi wa Bunju, Dar es Salaam, Robinson Olotho.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ndiye aliyeanzisha mpango wa kuwatumia mgambo wa JKT lengo likiwa ni kusaidia usimamizi wa sheria chini ya watendaji wa kata na mitaa kwa kuwa wao ndio wanaratibu shughuli zote za usimamizi wa usafi wakiwa chini ya watu wa mazingira wa wilaya na mkoa.

Akiwasomea hati ya mashtaka mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Mahira Kasonde, Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono, alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa moja la kusababisha majeraha.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 30, mwaka huu maeneo ya Bunju ambako walimpiga Robinson kwa kutumia rungu sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha.

Baada ya kusomewa kosa hilo washtakiwa hao walilikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Naye Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, alidai kuwa licha ya kesi hiyo kudhaminika lakini wanaiomba mahakama isubirishe dhamana ya washtakiwa hao kwa sababu kuu mbili.

Alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na suala la kiusalama na washtakiwa walionekana katika video zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari na kama watapatiwa dhamana usalama wao utakuwa shakani kwa sababu wananchi na ndugu wa mjeruhiwa watakuwa na hasira pia mjeruhiwa bado yupo hospitali na hali yake ya afya si nzuri.

Hakimu Kasonde alipowauliza washtakiwa hao kuhusu hoja hizo walidai kuwa suala la usalama wao liko vizuri na kuhusu hali ya afya ya mjeruhiwa walionana naye juzi na anaendelea vizuri na hayupo hospitalini.

Katika uamuzi wake, Hakimu Kasonde, alisema mahakama imekubali hoja za upande wa mashtaka kuhusu usalama wa washtakiwa hao hivyo wananyimwa dhamana hadi hapo itakapojiridhisha kuhusu usalama wao na kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 20, mwaka huu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles