Na Absalom Kibanda |
TULIHITIMISHA sehemu ya pili ya uchambuzi wetu wiki iliyopita kwa kueleza bayana kwamba, mafanikio na hatua kadhaa za msingi ambazo Rais John Pombe Magufuli anazichukua leo, kiini chake ni kazi iliyofanywa na watangulizi wake.
Kwa muktadha wa andiko hili, chimbuko la hoja ni kushiriki kwa namna ya kutoa maoni na mawazo ya mustakabali wa taifa katika zama hizi za Serikali ya awamu ya tano si kwa kulalamika au kuishia katika kukosoa na/au kusifia bali pia kuchambua japo kwa muhtasari mambo yaliyo nyuma ya pazia la kauli na uamuzi kadha wa kadha wa viongozi.
Chagizo muhimu ni angalizo la tahadhari si kwa Rais Magufuli na serikali yake tu, bali kwa taifa zima kuanza kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha misingi ya mafanikio, sambamba na kubadili mwelekeo pale kwenye maeneo ambayo yako bayana kwamba yanatuzamisha kama si kutukwamisha.
Pengine jambo kubwa ambalo tuliliona ni lile ambalo lilimfanya Rais Benjamin Mkapa wakati akimaliza muhula wake wa kwanza wa urais mwaka 2000 awe na uhakika wa asilimia 100 kwamba CCM ingemteua pasipo kusitasita au kujiuliza kuwa mgombea wake wa urais kwa kipindi cha pili.
Si hilo tu, Mkapa alikuwa amefanya kazi kubwa ambayo takwimu zake tulizibainisha ambayo ilikuwa ikimfanya awe na jeuri ya kutembea kifua mbele, akiwa na uhakika kwamba alikuwa pia anao uhakika wa kuibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2001.
Ni wazi kwamba pamoja na mafanikio ambayo yalionekana dhahiri kumbeba Mkapa wakati huo, kulikuwa pia kuna matukio mabaya, ya hovyo na pengine ya kuumiza ambayo yalikuwa yakiutia urais na serikali yake doa kwa kiwango cha kuitikisa taswira yake njema.
Kubwa katika hayo ilikuwa ni hali tete ya kisiasa ya Zanzibar ambayo msingi wake ulikuwa ni uhasama mkubwa wa kisiasa uliojengeka na uliozidi kushamiri kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho Mkapa alikuwa Mwenyekiti wake wa Taifa na Chama cha Wananchi (CUF).
Ni wazi kwamba, mafanikio ya Mkapa yalishindwa kumfunika shujaa wa siasa za mabadiliko Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na kimsingi, kiongozi huyo wa upinzani alionekana kubeba taswira iliyowazidi nguvu wanasiasa wote wa Tanzania waliokuwa ndani na nje ya CCM, ukimwacha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Ukiliacha doa hilo, Serikali ya Mkapa iliingia katika mtego na kubeba taswira mbaya ya kukosa ustahimilivu pale ilipofanya kosa ambalo hadi leo linaendelezwa na serikali za CCM la kuhoji uraia wa watu ambao kwa namna moja au nyingine wamejipambanua kuwa wakosoaji wakubwa wa mfumo wa utawala na uongozi wa nchi.
Katika hili, serikali ya Mkapa, ilimtangaza Jenerali Ulimwengu, mmoja wa wanahabari mahiri na wachambuzi adhimu wa masuala ya uongozi kuwa eti hakuwa raia wa Tanzania.
Uamuzi huo wa serikali si tu kwamba ulipingwa na kulaaniwa na wazalendo wengi, bali ulisababisha baadhi yetu kupatwa na shaka ambayo pengine haijapata kukoma vichwani mwetu iwapo kweli Rais Mkapa alikuwa anastahili kujipambanua kuwa mwanafunzi wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye urithi mama ulikuwa katika imani yake ya umajumui wa Afrika (panafricanism).
Hatua ya serikali ya Mkapa kumtangaza Ulimwengu, mtu ambaye amepata kuwa Mkuu wa Wilaya na kujipambanua kuwa Mtanzania ambaye uzalendo wake ulikuwa haujawahi kutiliwa shaka hata na Mwalimu Nyerere kuwa eti si raia, ulikuwa si tu jeraha (kwa Ulimwengu) bali pia usaliti wa misingi ya utaifa wetu.
Msimamo binafsi mkali wa Ulimwengu na ule wa magazeti aliyokuwa akiyaongoza wakati huo katika kuikosoa serikali ya Mkapa ndiyo ulioonekana dhahiri kuwa sababu ya msingi ya hatua hiyo ya kunyang’anywa fahari ambayo amekuwa akiifanya tunu kwa taifa ambalo wala sipati hata kigugumizi kusema analipenda na kulitumikia kwa dhati.
Ukakasi katika hatua hiyo ya serikali, ni ukweli kwamba, katika kampeni za mwaka 1995, Ulimwengu alijipambanua kwa maandishi na kwa kauli kumuunga na kumpigania kwa nguvu zake zote Mkapa wakati wa kampeni za urais pengine kuliko mwanahabari yeyote.
Hatua ya magazeti yake kukosoa utendaji kazi wa serikali hata kuchangia kwa kiwango kikubwa kujiuzulu kwa nyakati tofauti kwa mawaziri Dk. Juma Ngasongwa, Prof. Simon Mbilinyi na baadaye Dk. Hassy Kitine kabla ya mwaka 2000 kulimjengea taswira hasi Ulimwengu miongoni mwa watendaji katika taasisi za dola.
Sitaki kujifanya mtabiri bali naweza nikaandika kwa kujiamini kabisa kwamba, kama kuna doa ambalo lilichangia kwa kiwango fulani kupunguza ushawishi wa Mkapa wakati akielekea katika uchaguzi wa urais mwaka 2000, yalikuwa ni matendo ya namna hii.
Nimekuwa nikistaajabu kila ninapomsikiliza Rais Mkapa anapotaja mambo ambayo anafikiri anayajutia au kuyaona kuwa makosa aliyofanya yeye binafsi au na serikali au wasaidizi wake wakati akiwa Ikulu anapoacha pasipo kugusia hatua za hovyo za kuwapora watu stahiki yao ya uraia kwa kisingizio cha sheria.
Kwa baadhi yetu tunaojua kwa kusoma na kusikia juu ya Afrika ya wanamapinduzi akina Nyerere, Kwame Nkrumah na wenzao waliokuwa wakiamini kwa maneno na matendo juu ya Umajumui wa Afrika hata kuwapa haki ya uraia watu weusi wazaliwa wa Jamaica na Marekani tumekuwa tukijiuliza sana juu ya hatua za namna hii.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, kosa hilo la zama za Mkapa, lilirithiwa pia wakati wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na leo linaendelezwa kwa namna ile ile nyakati hizi za Rais Magufuli.
Ukiacha ukweli kwamba operesheni zinazogusa uraia wa baadhi ya watu ambao zimepata kuwatikisa kwa nyakati na vizazi tofauti vya uongozi si tu Ulimwengu bali pia Abdulrahaman Kinana, Iddi Simba, Hussein Bashe na wengine kadhaa, zimekuwa zikisababisha majeraha yasiyoisha vichwani mwa wengi.
Kama kuna jambo ambalo ninaweza kumshauri Rais Magufuli kwa dhati akalitazama na kulitafakari kwa kina kwa namna ile ile anavyofanya katika mambo mengine ya msingi basi ni hili la kuiangalia upya sheria ya uraia ambayo watendaji wenye nia ovu serikali wamekuwa wakiitumia kuumizia watu.
Nachelea kueleza kwamba, iwapo tutaacha hili likaendelea kutamalaki, iko siku huko tuendako watu walio na nia ovu watakuja kufanikiwa kupenyeza hoja hiyo dhidi ya kiongozi mkuu wa taifa au viongozi wa juu na kusababisha taharuki ambayo italifanya taifa lijutie dhambi hii ya fedheha ambayo imefumbiwa sana macho.
Ufedhuli wa kidola wa kuwabagua watu ama kwa uraia au rangi zao ndiyo ambao wakati wa Mkapa uliachwa ukakua sana kule Zanzibar na juhudi kubwa za makada wa CCM kuwatenga mahasimu wao wa kisiasa wa CUF kwa kuwatanabahisha na Waarabu au U Hizbu.
Matokeo ya ubaguzi huo ambao japo ulianza miaka mingi kabla ya Mkapa kuingia madarakani na kupata kukemewa sana na Baba wa Taifa ndiyo ambao umeendelea kuifanya Zanzibar kuishi katika kivuli batili cha umoja na mshikamano kilichoficha makovu na majeraha ya ubaguzi.
Ikumbukwe kwamba ni dhambi hii ya ubaguzi iliyolelewa na ikaachwa ikue, ilisababisha taifa hili mara mbili kwa miaka tofauti, mwaka 1985 na baadaye 2005 kumnyima urais aliostahili, mmoja wa wanadiplomasia na mwanasiasa mwenye rekodi iliyotukuka kitaifa na kimataifa, Dk. Salim Ahmed Salim. Hili nalo linahitaji mjadala unaojitegemea.
Hayo yote hata kama yako ambayo aliyarithi, ni sehemu ya mkwamo wa Mkapa ambao Rais JPM anapaswa kuutazama kwa jicho la tatu na kuukataa kata kata wakati anapoitekeleza ajenda yake ya ‘Tanzania Mpya’ ambayo mafanikio yake pamoja na mambo mengine yanapaswa kutibu majeraha ya kihistoria na yale ya hovyo..
Mkapa alikuwa na bahati ya mtende kwamba majeraha hayo hayakuweza kufua dafu mbele ya mafanikio yake makubwa kiuchumi yaliyorejesha matumaini na kumuingia muhula wa pili na akahitimisha hata urais wake 2005 kifua mbele kwa Tanzania Bara na akajikuta akipata fedheha kule Zanzibar mwaka 2000 -2001.
Japokuwa mwaka 2000 alipanda kwa kura na kufikia asilimia 71 kulinganisha na 61 za mwaka 1995 kama tulivyochambua wiki iliyopita, kule Zanzibar hali ilikuwa mbaya na kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 ulioshuhudia mpasuko mkubwa, Tanzania ilizalisha wakimbizi wa kisiasa.
Akiwa Mwanadiplomasia kihistoria, Mkapa alifedheheka na ili kufuta jeraha hili, akaalikwa aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chief Emeka Anyaoku kuja kusuluhisha mgogoro mkubwa wa kisiasa ambao chimbuko lake ni hulka ya kupuuzia mambo.
Hatua ya kumuita Chief Anyaoku ilimrejeshea Mkapa imani iliyopata doa kubwa katika jumuiya ya kimataifa ambayo ilifuatiwa na hatua ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB), kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania.
Mwaka mmoja tu baada ya uchaguzi wa mwaka 2000, taasisi hizo ziliingiza Tanzania katika kundi la nchi maskini zenye madeni yasiyolipika ambazo hata hivyo sera za fedha za serikali zilionesha kusimamia uchumi vyema lililojulikana kwa kifupi HIPC na mwaka huo huo, kiasi cha deni la zaidi ya dola za Marekani bilioni mbili kikafutwa.
Hadi alipokuwa akielekea kumaliza kipindi chake cha urais mwaka mmoja kabla (2004), Mkapa alikuwa amefanikiwa kushusha mfumuko wa bei hadi asilimia nne huku ukuaji wa pato la taifa ukifikia asilimia 6.7.
Mafanikio hayo yalisababisha wakati huo huo akiba ya fedha za kigeni kupanda hata kuwa ni ile iliyokuwa ikifikia kiwango cha thamani za bidhaa za miezi minane zilizokuwa zikiagizwa kutoka nje.
Mafanikio hayo ya kitakwimu ya Mkapa japo yalizidisha matumaini na kuua nadharia ya ukapa yalikabiliana na changamoto kubwa ya kiukinzani kutoka kwa wachambuzi ambao baadhi yao waliyaponda kwa kutoakisi maisha halisi ya Watanzania walio wengi.
Hata hivyo, Mkapa aliondoka madarakani akiwa kifua mbele kwa kuongeza wigo wa ajira na uwekezaji kwani kilikuwa ni kipindi chake ambako kampuni takribani zote kubwa za simu ziliingia nchini na kusisimua uchumi.
Ni kipindi hicho hicho ambacho sekta za madini na utalii zilianza kuchuana katika kuchangia pato la taifa kwani ndiko pia kampuni za kimataifa za madini zilipoanza.
Kama kuna jambo lilimpa jeuri Mkapa ni namna alivyounda serikali madhubuti akiteua watu wenye uwezo mkubwa kuongoza wizara ambazo zilichangia uchumi, uwekezaji, madini, maliasili na utalii.
Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana Mkapa alikuwa akipatwa na simanzi kubwa kila wakati wapinzani wake waliokuwa ndani na nje ya serikali yake walipoibua mashambulizi na kashfa, baadhi zikiwa ni za kufinyanga ambazo zilimpotezea majemedari wake kadhaa wa kazi.
Ingawa ni kweli kwamba, aliwaamini mawaziri wake wengi waandamizi na kuwaacha wakifanya kazi kwa kujiamini katika maeneo aliyowapangia kazi pasipo kuwahamisha hamisha, alikuwa dhaifu kukabiliana na kashfa na tuhuma walizoelekezewa hata baadhi yao kulazimika kujiuzulu.
Udhaifu huo wa Mkapa ulirithiwa pia na Kikwete ambaye naye alipoteza mawaziri kadhaa akiwamo Waziri Mkuu wake Edward Lowassa katika mazingira ya namna hiyo.
Katika hili eneo, ni mapema kwa sasa kulipima ipasavyo kwa JPM japokuwa, katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya mwanzo anaonekana kuwa na udhaifu ulioacha mapengo, mengine makubwa katika uteuzi wa mawaziri wake.
Ukiwaweka katika mizania si ya usomi tu bali hata ile ya umahiri na umakini mawaziri wengi wa JPM utawapata wachache sana wa kariba ya kina Dk. Abdallah Kigoda, Daniel Yona, Prof. Simon Mbilinyi, Prof. Mark Mwandosya, Iddi Simba, Zakhia Meghji, Magufuli (waziri wa Ujenzi) na Lowassa (Waziri wa Maji).
Ni wazi washauri waliokuwa wakimsaidia Mkapa katika uteuzi wa wasaidizi wake, pamoja na upungufu mwingi uliopata kuitikisa serikali yake, walimsaidia sana Rais kutimiza wajibu wake, ukilinganisha ilivyo leo ambako Rais mwenyewe ndiye anayeonekana kuwa waziri kwenye wizara nyingi.
Tutalitafakari hili la mawaziri wa JPM wiki ijayo….