WATAHINIWA 960,000 KUFANYA MTIHANI DARASA LA VII KWA MFUMO MPYA

0
998Na ELIZABETH HOMBO,DAR ES SALAAM

WATAHINIWA 960,202 wanatarajiwa kuanza Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) leo, huku Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) likionya  watakaofanya udanganyifu watachukuliwa hatua kali za sheria.

Mtihani huo ambao utafanyika leo na kesho nchi nzima, muundo wake umebadilika kwa wahitimu kujibu maswali ya kuchagua na yale ya kujieleza tofauti na uliopita ambao maswali yote yalikuwa ya kuchagua.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alisema kati ya watahiniwa hao 960,202, wasichana ni 503, 972 (asilimia 52.49) na wavulana ni 456,230 (asilimia 47.51).

Alisema watahiniwa wasioona waliosajiliwa ni 90, wasichana 31 na wavulana 59, wenye uoni hafifu ambao wanahitaji maandishi makubwa ni 846, wavulana 475 na wasichana 371.

“Baraza linatoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kufanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu, wasimamizi wote wanaaswa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu.

“Baraza pia linawataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani.

“Hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha   mtihani huu,”alisema Dk. Msonde.

Alisema baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajiridhisha kuwa kuwapo kwake kunahatarisha usalama wa mitihani ya taifa.

“Pia watahiniwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya udanganyifu watafutiwa matokeo yao yote kwa mujibu wa kanuni ya mitihani.

“Wadau wote wanaombwa kutoa taarifa katika vyombo husika kila wanapobaini mtu au kikundi cha watu kujihusisha na udanganyifu wa mitihani wa aina yoyote ile,”alisema Dk. Msonde.

Kuhusu muundo huo mpya, Dk. Msonde alisema hiyo ni baada ya baraza kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu wakitaka yawepo maswali ya kuchagua na yasiyo ya kuchagua.

“Mtihani uliopita wa mwaka 2017, maswali yote yalikuwa ya kuchagua lakini kuanzia mwaka huu kila somo litakuwa na maswali 45, kati ya hayo 40 yatakuwa ya kuchagua na matano yasiyo ya kuchagua,”alisema.

Mfumo wa mitihani ya kuchagua ulianza mwaka 2012 huku ukipingwa na wadau mbalimbali wikiwamo wabunge wakisema utazalisha wahitimu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Mfumo huo ulishuhudia nusu ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 wakiwa wamepata asilimia 40 ya alama kwenda chini.

Waziri wa Elimu wa wakati huo, Dk. Shukuru Kawambwa akitangaza matokeo hayo Desemba 2012, alisema wanafunzi 294,833 (asilimia 52.58) waliopata daraja D walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Idadi hiyo iliungana na wenzao 265,873 waliopata madaraja ya A,B na C (asilimia 47.41).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here