Na Maregesi Paul, Mtwara
SIKU chache baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, kusema yeye ndiye tumaini la Watanzania baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamemjia juu.
Wakizungumza na MTANZANIA Jumatatu kwa nyakati tofauti juzi wabunge hao walisema, Sumaye hana sifa za kusema ndiye tumaini la Watanzania kwa sababu ni kati ya mawaziri wakuu walioiharibu nchi.
Katika maoni yake, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, alisema alishangazwa na kauli hiyo ya Sumaye kwa kuwa ndiye kati ya mawaziri wakuu wastaafu wasiotakiwa kushika wadhifa wowote katika nchi hii.
“Mimi nilishangaa niliposikia amesema eti yeye ndiye tumaini la Watanzania na huku akiwashutumu baadhi ya viongozi kwamba wanataka teni percent katika miradi ya Serikali.
“Wakati nikishangaa, kuna watu wakanipigia simu kuniuliza kama kweli hiyo ni kauli ya Sumaye aliyewahi kuwa Waziri Mkuu au ni majina tu ya ukoo yanafanana.
“Nikawaambia ndiye huyo huyo aliyekuwa waziri mkuu na ndiye huyo huyo aliyeifikisha nchi pabaya.
“Sasa namwambia Sumaye, kaa kimya, mambo yako tunayajua mengi sana, usifikiri Watanzania ni wajinga, usifikiri wana CCM hawakujui.
“Yaani huyu jamaa yeye enzi zake alishindwa hata kukamata wezi wa shilingi 5,000 lakini sasa anaibuka na kusema ndiye tumaini la Watanzania, nashukuru kwamba ameanza kujianika mapema ili na sisi tupate muda wa kukabiliana naye.
“Hatukubali kuongozwa na viongozi wa aina ya Sumaye, hatutaki kabisa na wana CCM wezangu nawaambia huyu mtu anataka kutuharibia chama, yaani sisi tunataka rais mchapakazi halafu naye anaanza kutikisa kiberiti ili aone kama kimejaa, nakwambia hataweza,” alisema Kangi.
Kwa mujibu wa Kangi, baadhi ya matatizo yanayolikabili Taifa yalianzia katika utawala wa Sumaye na kwamba alishindwa kukabiliana nayo kwa sababu hana uwezo wa kuongoza.
Kutokana na hali hiyo, alisema atafanya kila linalowezekana kuhakikisha viongozi wa aina ya Sumaye hawapati nafasi ya kuongoza nchi hii kwa vile wakipata tena nafasi hiyo watazidi kuwadidimiza Watanzania.
Wakati Kangi akisema hayo, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, alisema aliposikia kauli hiyo ya Sumaye hakuamini hadi alipoithibitisha kupitia vyombo vya habari.
“Mwanzoni watu waliponiambia habari zake nilishtuka na sikuamini mara moja, lakini nilipofuatilia vyombo vya habari nikathibitisha kwamba ndiye aliyesema kwamba ni tumaini la Watanzania.
“Kwa maana hiyo nami nasema, aondoe kabisa kichwani mwake ndoto alizonazo kwa sababu kati ya viongozi wasiotakiwa kuongoza nchi hii ni yeye.
“Yaani huyu jamaa anataka kutufanya Watanzania ni wajinga, namuomba sana asipoteze muda wake na kama anaweza aende akalime mashamba yake kwa sababu nasikia anayo mengi sana na kama hawezi kulima, basi atulie aendelee kula NSSF yake,” alisema Filikunjombe.
Alisema baada ya kupata uhakika na kauli hiyo kwamba ilitolewa na Sumaye, alimtafuta Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa njia ya simu ili amweleze mambo ya kufanya dhidi ya Sumaye.
“Nilimtafuta Pinda ila kwa bahati mbaya nikaambiwa yuko Uingereza na lengo kubwa la kumtafuta nilitaka nimwambie aangalie nyumbani kwake kama kuna kitu chochote kilichoachwa na Sumaye akichukue ampelekee.
“Nilitaka nimwambie aangalie hadi kwenye vyumba vya watoto ili kuona kama kuna kitu chake na kama asipokipata, akaangalie na kule ofisini kwake na ikibidi apekuepekue mafaili aangalie kama kuna kitu kilisahaulika ambacho anataka kukirudia,” alisema Filikunjombe.
Naye Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy, aliwataka Watanzania wampuuze Sumaye kwa kuwa hana jipya atakalolifanya hata akipewa nafasi nyingine ya uongozi.
“Huyu achana naye kwa sababu ukiwa na viongozi wasahaulifu kama yeye ni hatari sana katika Taifa. Yaani mara hii tu ameshasahau kwamba ndiye aliyeharibu nchi hii?
“Hivi hakumbuki alivyoshiriki kuuza majumba ya Serikali? Hivi hakumbuki alivyoshiriki kuiangamiza Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Kilombero Sugar?
“Kama anafikiri Watanzania tumelala, namwambia hatujalala, tuko macho na tuna kumbukumbu zetu kama kawaida na hapati kitu hata kama anakitaka,” alisema Kessy.