26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 3, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUM- 3: Mashitaka ya Ballali

Aliyekuwa Gavana wa BOT Daudi Balali
Aliyekuwa Gavana wa BOT Daudi Balali

Na Waandishi Wetu

MASHITAKA dhidi ya marehemu Daudi Ballali kama yalivyoitwa na wadadisi na wafuatiliaji wa mambo, yaliandaliwa na wabunge wa kambi ya upinzani na baadhi ya vyombo vya habari katika mfumo wa maswali tata ambayo mtu pekee aliyekuwa na majibu yake sahihi alikuwa ni yeye mwenyewe Ballali.

Maswali hayo yalitokana na kashfa ya wizi wa mabilioni ya fedha yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo iliibuka kwa nguvu ndani ya Bunge la Jamhuri mwishoni mwa mwezi Juni na mwanzoni mwa Julai mwaka 2007.

Kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) ambazo MTANZANIA limeziperuzi, zinaonyesha kuwa wabunge wa kambi ya upinzani ambao walikuwa wachache bungeni, walifanikiwa kwa kiwango kikubwa kiliteka Bunge kutokana na uking’ang’anizi waliouonyesha wa kutaka kashfa hiyo ichunguzwe na majibu ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani.

Kwa maana nyingine, matakwa hayo ya wabunge wa upinzani yalichukuliwa na wengi kuwa ilikuwa ni namna ya kumlazimisha marehemu Ballali ajitokeze hadharani kuizungumzia kashfa hiyo, kutokana na kile kilichokuwa kikiaminika kuwa ndiye pekee aliyekuwa akijua undani wa wizi huo.

Hili linadhihirishwa na maelezo ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, ambaye alikuwa kinara wa mapambano hayo na mmoja wa wale waliomtuhumu kwa namna inayotafasiriwa vile vile na wadadisi kuwa ni kumshitaki bungeni marehemu Ballali.

Baadhi ya maelezo hayo ya Dk. Slaa ni yale aliyoyatoa katika hotuba yake aliyoisoma kwa niaba ya kambi ya upinzani bungeni kuhusu makadirio ya matumuzi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2007/2008.

Katika hotuba yake hiyo alimtuhumu marehemu Ballali kuwa kwa wadhifa wake wa Gavana wa Benki Kuu alizembea au alihusika moja kwa moja na matumizi mabaya ya fedha za Serikali ndani ya taasisi nyeti kwa uchumi wa taifa aliyokuwa akiiongoza.

Pia, Dk. Slaa alimtuhumu mke wa marehemu Ballali, Ana Muganda kuwa ni mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya ‘Time Mining’ na pia ni mwanahisa wa Kampuni wa Run Gold ambayo iliuziwa Kampuni ya Meremeta.

Aidha, Ballali alituhumiwa kuwa na uraia wa nchi mbili, Tanzania na Marekani na kwamba alikuwa akilipwa mishahara miwili na tuhuma nyingine aliyokuwa akishutumiwa nayo ni kujihusisha na ubadhirifu wa majengo ya BoT ambazo enzi hizo yalikuwa bado yakijengwa.

Katika mahojiano yake ya hivi karibuni na MTANZANIA kuhusu utata ilioghubika kifo cha Ballali, Dk. Slaa alisema bado anaamini marehemu huyo ndiye mtu pekee aliyekuwa na ushahidi wa kutosha uliokuwa ukihitaji kuwatia mbaroni wale wote waliohusika na wizi wa fedha za EPA hivyo Serikali kushindwa kumfikia alipokuwa mgonjwa kitandani nchini Marekani na kuchukua ushahidi wake kunajenga mazingira yenye utata wa kashfa nzima.

Uchunguzi wa MTANZANIA kwenye makabrasha ya Bunge na katika kumbukumbu rasmi za Bunge unaonyesha kuwa, hali ilianza kuchafuka ndani ya ukumbi wa Bunge mwezi Juni, 2007, baada ya Dk. Slaa ambaye alikuwa Mbunge wa Karatu kutangaza nia ya kutaka kuwasilisha hoja binafsi mbele ya Bunge ya kutaka iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kashfa hiyo.

Mmoja wa watumishi wa Bunge wa kitengo cha uandaaji wa kumbukumbu rasmi za Bunge aliyefikiwa na MTANZANIA na kuhojiwa kuhusu hali ilivyokuwa wakati wa sakata hilo, alisema mwangwi wa kishindo cha kashfa ya EPA utaendelea kuvuma bungeni kwa muda wa miaka mingi na jina la Dk. Slaa na marehemu Ballali hayatafutika katika kumbukumbu rasmi na zisizo rasmi za Bunge.

“Hakuna kitu kidogo hapa duniani, Dk. Slaa alipoanza walimdharau lakini baadaye walikuja kuona athari zake. Marehemu Ballali atabaki katika kumbukumbu rasmi na zisizo rasmi za Bunge nakuambia kaka. Ni sawasawa na wewe kaka jinsi ambavyo maandishi yako yatadumu kwa miaka mingi.

Kati ya Juni na Julai 2007, Bunge lilikuwa kwenye wakati mgumu sana, wakubwa walikuwa hawalali kwa sababu ya kashfa ya EPA.

Bunge ambalo liliahidiwa kuletewa majibu ya uchunguzi wa wizi wa fedha za EPA halijapelekewa hadi sasa na kile ambacho kiliitwa mashitaka ya marehemu Ballali kilibaki hewani kwa sababu alikufa na majibu yake moyoni. Endelea kuangalia unachotafuta kaka ukimaliza uniruhusu nikafanye mambo mengine.” Alisema ofisa huyo ambaye jina lake linahifadhiwa.

Kumbukumbu zaidi za Bunge ambazo MTANZANIA liliziperuzi zilionyesha kuwa katika mkutano wa nane wa Bunge, Serikali ililazimika kutoa tamko la kuanzisha uchunguzi wa wizi katika akaunti hiyo ambao ulikuwa ukifanywa na vyombo vya dola.

Akitoa tamko hilo Bungeni, aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa, alisema kuwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha dhidi ya Benki Kuu zilizotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2007/2008 zimeishtua na kuikasirisha Serikali.

Wabunge waliochangia hoja hiyo kwa mujibu wa kumbukumbu hizo ni pamoja na Dk. Slaa, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya na aliyekuwa Mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe.

Kumbukumbu za Hansard za mkutano wa nane, kikao cha kumi kilichoketi Julai 2 mwaka 2007, katika sehemu moja ambayo Waziri Mkuu anajibu hoja za Bunge inasomeka: “Tumechukizwa na kushtushwa na taarifa kwamba kuna fedha zimepotea ndani ya Benki Kuu.

Kwa hiyo baada ya kuchukizwa na jambo lenyewe tumemwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), tunamwamini ni mtu shupavu, ashirikiane na ‘audit’ za kimataifa wakague benki wajue imekuwaje jambo hili kama ni kweli.

Je ni kweli? Nani anahusika? Ni akina nani na tuchukue hatua gani ili jambo hili lisije likatokea tena kama ni kweli limetokea.

Kwa hiyo Serikali tumechukua hatua kabla ya kuja hapa. Nilikuwa nawasihi wenzangu wa upinzani, Hamad Rashid na Willbrod Slaa kwamba jambo hili halihitaji Kamati Teule.

Lakini si hivyo tu, tumeshirikiana na kushauriana na wafadhili wetu wanaotusaidia katika miradi pamoja na IMF juu ya utaratibu wa kufanya kuhusu jambo hili na utaratibu tuliokubaliana ni huu wa kumteua CAG na kutafuta wakaguzi wa kimataifa kufanya kazi hii. Tunadhani huu ni utaratibu muafaka.

Baada ya taarifa hiyo kupatikana tutachukua hatua zinazopaswa na Bunge hili litaarifiwa.

Lakini la pili Benki Kuu ni roho ya uchumi wa nchi. Si chombo cha hivi hivi. Hata kama inawezekana mambo yenyewe labda yametokea kweli, sijui sina hakika na mimi lakini tujue kwamba Benki Kuu hii ni moja ya Benki Kuu zinazokubalika hapa Afrika kwa kazi nzuri.

Tujue Benki Kuu hii imechangia sana katika mabadiliko ya uchumi yanayoendelea ndani ya nchi yetu. Tujue ndani ya Benki Kuu ile wapo vijana wanawake na wanaume wanaofanya kazi kwa makini na vizuri sana.

Kwa hiyo tusiwahukumu wote kwa pamoja lakini tuseme jambo hili tumeliona, tunalichukulia hatua.

Hatuna haja ya kamati, tutasaidiana kutoa taarifa wakati huo nini tumefanya baada ya kupata taarifa kamili.” Inasomeka hivyo sehemu ya taarifa ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Lowassa.

Hata hivyo, tamko hilo lilipingwa na wabunge wa upinzani waliotaka Bunge lichukue jukumu la kufanya uchunguzi badala ya kuachia taasisi nyingine kwa hofu ya ukweli kufichwa.

Ni mwenendo huo mjadala wa wizi wa fedha katika akaunti ya EPA uliokuwa ukiendelea kwenye vikao vya Bunge ndio ambao hatimaye ulimuibua marehemu Ballali na kuitisha mkutano na waandishi wa habari, ambapo pamoja na kuzungumzia mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa taifa na mfumuko wa bei aliitumia pia nafasi hiyo kujibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake binafsi na taasisi aliyokuwa akiiongoza ya Benki ya Tanzania.

Katika mkutano huo uliofanyika ofisini kwake BoT mwezi Julai 2007, Ballali alikanusha kuhusika kwa namna yoyote na wizi huo na kwa maneno yake mwenyewe alisema: “Watanzania ni wanyonge kifikra na wamekosa uzalendo wa nchi yao ndiyo maana wameruhusu baadhi ya watu kufanya ubadhirifu.

Ubadhirifu huu ni moja ya matatizo yanayojitokeza dhidi ya hali ya uchumi wa nchi. Tuhuma zote dhidi ya BoT na mimi binafsi si za kweli na zimeathiri mtazamo wa watu wengi kwa kiwango ambacho sikukitarajia.

Taarifa iliyotolewa kwenye intaneti ni uongo mtupu tena haina jina halisi la mwandishi. Inaonekana kuna watu wanagombana au wanagombea kitu na mwandishi wa taarifa hiyo anaonekana si mzalendo na mchoyo.

Siwezi kujiuzulu wadhifa wangu kwa sababu hizi ni tuhuma tu. Tuhuma tu hazitoshi lazima kuwe na substance (maelezo ya uhakika) ya ukweli ndani yake, la sivyo watu watakuwa wanatuhumiwa tu ili waache kazi.”

Hiyo ilikuwa ni sehemu ya kauli ya Ballali mwenyewe kama ilivyonukuliwa na baadhi wa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo wakati akizungumzia kashfa ya wizi wa EPA na hatima ya ajira yake ndani ya BoT.

Hata hivyo, maelezo hayo hayakusaidia kupoza hali ya hewa iliyokwishachafuka kwani wapinzani chini ya Dk. Slaa walizidi kumuandama na huku wakiwatuhumu baadhi ya viongozi wa Serikali kuhusika katika kashfa hiyo.

Katikati ya mwendelezo wa kelele hizo za Dk. Slaa na wenzake kwa upande mmoja na vyombo vya habari kwa upande mwingine, marehemu Ballali aliitwa bungeni Dodoma ambako ili kujua kilichotokea endelea kufuatilia ripoti hii maalumu ambapo kesho Dk. Slaa atafichua kilichokuwa kimejificha nyuma ya kivuli cha marehemu Ballali.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles