28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Kikwete awaangukia Ukawa

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

Pendo Fundisha, Mbeya na Hadia Khamis, Dar es Salaam

RAIS Jakaya Kikwete amewaangukia Wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kurejea katika Bunge Maalumu la Katiba kushiriki mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

Aidha, amewataka maaskofu na viongozi wa dini nchini bila kujali dini zao kuwaombea Ukawa ili kuondokana na mapepo yanayowasababishia kususia vikao vya Bunge hilo.

Wakati Rais Kikwete akilazimika kulizungumzia suala hilo katika Maadhimisho ya miaka 75 ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) yaliyofanyika jijini Mbeya baada ya Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali, kumuomba kuingilia kati suala la mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alishawahi kulizungumzia bungeni na katika mikutano mara kadhaa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania waliotoa tamko la kuwataka Ukawa kurejea bungeni bila masharti.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja ikiwa ni miezi minne sasa tangu Ukawa watoke bungeni bila kuonyesha msimamo wa kurudi kuendelea kujadili rasimu ya Katiba Mpya hadi leo hii.

“Nimefarijika kusikia nanyi viongozi wa dini mkiwasihi wajumbe hawa ambao waliondoka bungeni kurejea kwa kuwa  matumaini yetu sisi wote ni kumalizika kwa kazi hii ambayo kwa asilimia kubwa tayari imemalizika.

“Katiba Mpya imelenga kuondoa au kumaliza kasoro ndogo ndogo zilizomo katika Katiba ya awali inayotumika sasa, hivyo ni vema wajumbe wakaliona hilo na kuwatendea haki wananchi ambao wanawawakilisha.

“Lengo la Watanzania ni kupata Katiba itakayotekelezeka, itakayodumisha upendo, amani na utulivu, Katiba itakayochochea maendeleo na itakayolinda haki za msingi za wananchi hivyo ni vema mchakato huo ukakamilika kwa wakati ili jamii ya Watanzania ifaidike na matunda haya.

“Katiba ya nchi ni Katiba ya Watanzania wote kwa ujumla, hivyo ni vyema viongozi wa vyama vya upinzani kutumia busara hiyo ili kurudi bungeni kuendelea kuijadili Katiba hiyo.

“Sisi sote tuna wajibu wa kuwahudumia wanakondoo, lakini mwanakondoo huyo lazima awe na imani ndipo apate kuokoka, kwa vile viongozi wa dini mna heshima kubwa kwa Taifa na katika suala zima la kuitangaza injili naomba muitumie fursa hiyo kuwaombea viongozi hawa ili warudi bungeni waweze kukamilisha kile tulichowaagiza,” alisema Rais Kikwete.

Alisema anashangazwa na ukimya wa viongozi hao kwa kuwa hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa Ukawa aliyetoa tamko la kurudi bungeni kuendelea na mchakato wa kujadili Rasimu ya Katiba Mpya wala kutoa masharti ya nini kifanyike.

“Mara nyingi mtu anapogoma anakuwa na sababu maalumu na masharti kwamba ili nirudi basi lazima nitekelezewe moja, mbili au tatu lakini kwa wenzetu hawa hakuna aliyetoa tamko la aina hiyo hadi sasa, sijui hatima yao ni nini.

“Inawezekana kuna pepo lililoingia katika utoaji wa maoni ya mmoja mmoja na lazima yapite maombi ili kulikwamua hilo pepo hapa, kwa sababu viongozi hawa walipishana Kiswahili na ndiyo kimetokea kilichojiri,” alisema Rais Kikwete.

Alisema yeye na wenzake walibuni rai ya kujadiliwa kwa rasimu ya Katiba Mpya ili kupata Katiba iliyo bora kuliko iliyopo sasa.

“Wajumbe wenyewe ndio walikubaliana kujadili sura hizo kwa siku 14 katika maoni ya wengi waliwasilisha vizuri lakini maoni ya mmoja mmoja yaliingiliwa na pepo lililovuruga hali ya hewa bungeni hali iliyosababisha baadhi ya wajumbe kuamua kususa,” alisema Rais Kikwete.

Alisema ni vyema wajumbe hao kukaa pamoja ili kujua uamuzi wa muundo wa Serikali wanaoutaka kama ni mbili au tatu.

Alisisitiza maombi ya Watanzania ndiyo yatakayoweza kuwashawishi viongozi wa Ukawa kurejea bungeni Agosti 5, mwaka huu ili kufanya kazi waliyotumwa.

Aliwataka viongozi wa dini kuwa makini na watu wasiopenda amani ya nchi wanaotumia miamvuli ya injili kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles