Na CHRISTIAN BWAYA
SHULE ni eneo mojawapo muhimu katika malezi ya watoto. Pamoja na mambo mengine, shule inapanua wigo wa urafiki kwa mtoto. Shuleni ndipo mahali ambapo mtoto hukutana na wenzake waliotoka kwenye mitaa tofauti na kule alikokulia. Kupitia wenzake anaweza kujifunza mambo ambayo kwa sababu moja au nyingine hakujifunza nyumbani kwao.
Ukiwachunguza watoto unaweza kugundua kuwa kuna mambo mazuri wanajifunza kwa sababu tu walipata nafasi ya kufahamiana na wenzao wanaotoka kwenye familia zenye desturi tofauti na kule walikokulia wao. Mfano kama mtoto hakufundishwa kuwaelewa wenzake, shule inaweza kumlazimisha kujifunza kuvaa viatu vya wenzake. Kupitia michezo na wenzake, atajifunza kuwa kuna wakati analazimika kutazama mambo kwa macho yao.
Ukiacha watoto wenzake, shuleni mtoto hukutana na watu wazima wanaoweza kuwa na sauti kubwa kuliko wazazi wake. Hapa kuna walimu wanaomfundisha, walezi wanaomhudumia akiwa kwenye mazingira ya shule na wakubwa zake wanaosoma madarasa ya juu. Watu hawa, kila mmoja kwa sehemu yake, wanaweza kupata mafunzo mapya mazuri ambayo mtoto hajawahi kuyapata akiwa nyumbani.
Ikiwa mtoto hajawahi kufundishwa kuheshimu wakubwa, shuleni atakumbushwa wakati mwingine kwa adhabu. Ikiwa hakufundishwa kujitegemea, shuleni atalazimika kushika hiki na kile na atajifunza shughuli za mikono.
Kwa upande mwingine, kutegemea na mahali iliko shule, iko hatari ya mtoto kujifunza mambo yanayokwenda kinyume na matarajio ya wazazi na jamii kwa ujumla. Watoto anaosoma nao, wanaweza kuwa na tabia za ajabu ambazo mtoto bila kujielewa atajikuta anaziiga. Tunafahamu, kwa mfano, watoto hujifunza lugha isiyo ya kistaarabu wakiwa shuleni. Mtoto anaweza kutoka kwenye familia iliyomfundisha mambo ya adili lakini mazingira ya shule yakamfunza tabia zisizokubalika.
Vile vile kuna uwezekano wa mtoto kukutana na watoto wengine waliokulia kwenye mazingira yaliyowazoesha ubabe na matumizi ya nguvu. Hawa wanaweza kumtukana, kumzomea na wakati mwingine kumdhalilisha kwa sababu tu yuko tofauti na wao. Mazingira kama haya yanaweza kumwathiri mtoto kisaikolojia. Kwa mfano, wapo watoto wanaopoteza hali ya kujiamini kwa sababu tu ya kuchekwa na watoto waliokutana nao shuleni. Ni muhimu kwa mzazi kuwa karibu na mtoto ili kumwepusha na ujumbe hasi unaopenyezwa kwake akiwa shuleni.
Vile vile, tukumbuke kuna sauti ya mwalimu. Kwa kuwa huyu ndiye anayemfundisha mtoto hesabu, kusoma na kuandika, basi huamini kile anachokisema mwalimu ndio ukweli. Bila shaka umewahi kumwambia mwanao kitu akakubishia kwa sababu mwalimu wake hakumwambia hivyo. Tafsiri yake ni kwamba kile anachokisema mwalimu kinaweza kuwa na nguvu ya kuamua mtoto atajitazamaje na atawaonaje wenzake.
Katika mazingira kama haya, fikiria mwalimu huyu anasema maneno yanayomwuumiza mtoto. Maneno kama, “Lioneni halina akili,” “Mchekeni huyo,” “Mzomeeni hajui hesabu” na maneno yanayofanana na hayo yanaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wake. Tunafahamu, kwa mfano, wapo walimu waliowahi kutudhalilisha kwa maneno tukiwa wadogo na bado tunayakumbuka matusi hayo hadi leo hii.
Mwalimu anaweza kuzungumza maneno fulani kama utani lakini ufahamu wa mtoto ukayaamini. Ndio maana tunasisitiza walimu kuwa makini na lugha wanazotumia wanapokuwa na watoto. Mzazi, kwa upande mwingine, anahitaji kufuatilia kwa karibu uhusiano uliopo kati ya mtoto na walimu wake.