|Waandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwanyembe, amezitaka kampuni za visimbuzi za DSTV, Azam na Zuku kwenda kwenda Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wapewe utaratibu wa kurusha chaneli za ndani za bure kama wamevutiwa na soko hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Jumanne Agosti 14 Mwakyembe amesema licha ya mikataba ya kampuni hizo kutoruhusha kurusha chaneli hizo lakini wamekuwa wakizirusha na kuwatoza wananchi gharama ili kuzipata.
“Kama hawa wenzetu wana hamu sana na soko hili la ndani wasitumie njia za chini chini waende TCRA wapewe utaratibu wa namna wa kuupata,” amesema Mwakyembe.
Alizitaja baadhi ya chaneli ambazo zinapaswa kupatikana bure kupitia visimbuzi mbalimbali ni pamoja na TBC, Star TV, ITV, Channel Ten na EATV na kusisitiza kuwa TBC ni lazima irushwe na kila kisimbuzi bila malipo yoyote.
Dk. Mwakyembe amesema pamoja na ufafanuzi mzuri uliotolewa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ameamua kulitolea ufafanuzi jambo hilo ili kuondoa sintofahamu kwa wananchi.
“Naomba nianze kwa kutamka kwamba maelezo yote yaliyotolewa na Waziri Isack Kamwelwe yanawakilisha majibu ya wizara yangu,” amesema.
Dk. Mwakyembe pia amesisitiza kuwa serikali haijafuta leseni za visimbuzi vya Azam, Zuku na Multichoice Tanzania bali wanawataka kuondoa chaneli ambazo zinatakiwa kurushwa bure kulingana na matakwa ya mikataba yao.