27.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

MAONYESHO YA KILIMO YAFANYIKE WILAYANI

 


na Shermarx Ngahemera

NI kweli kabisa kwamba, kuona ni kuamini  kwani Maonyesho ya Nanenane yamekamilika ambapo taasisi nyingi zinazoshughulika na kilimo, wafanyabiashara wa bidhaa za pembejeo za kilimo na watafiti wa shuguli hizo, walipata fursa ya kuzipeleka na kutoa maelezo ya shughuli zao mbalimbali. Shukurani kwa wote!

Kwa kifupi shughuli zilikwenda vizuri  kwani wenyeji wa mwaka huu walikuwa Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya mikoa ya Mashariki ya Ziwa ikiwamo Shinyanga, Geita na Simiyu kwa pamoja walionesha juhudi zao kitaifa pale Bariadi kwenye viwanja vya Nyakabindi. Hongera kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, kwa matayarisho na zoezi zima la maonyesho kwani wote waliofika wanasifia maandalizi na ukarimu wa waandaaji.

Lakini kuna haja ya kulitazama zoezi hilo  la maonyesho kwa maana ya kuliboresha ili kuzuia  nguvu kubwa inayotumika kupotea kwani  kuna mapungufu ya sehemu (location) yanapofanyika  na hadhira  yake, kwani inaonekana unaishia kama mchezo wa kuigiza ambao unafurahisha  au kuhuzinisha, lakini hauna athari kubwa kwa watazamaji hao kwa kukosa uhusiano wa moja kwa moja.

Ilivyo sasa maonyesho hayo ni ya wakulima kwa jina tu lakini hadhira yake ni wafanyabiashara na wafanyakazi ambao ni maofisa wa mkoa husika na taasisi mbalimbali za Serikali na ni mjini. Wakulima halisi wako vijijini na maonyesho yako mijini kilomita zaidi ya mia toka anakoishi mlengwa. Hii ni kasoro inayotaka marekebisho ya haraka na tuache kutumia  fedha za wakulima kwa kuwapa kilemba cha ukoka kuwa maonyesho kuwa ni yao; wakati sio!

Mahali karibu kwao na kwenye maana ni wilayani  na si mkoani kwani hapo ni muhimu kwa watawala tu na si wakulima. Hivi basi, tunampigia mbuzi gitaa na muziki mzuri lakini hawezi kuucheza.

Kwa mtazamo huo, ningeshauri kuwa maonesho hayo yafanyike kwa mzunguko kila wilaya katika mkoa husika mwaka hadi mwaka ili kupeleka teknolojia na elimu ya kilimo, ikiwamo ya ufugaji, uvuvi na kilimo biashara. Hivyo, kuleta mabadiliko haraka kwani  wakulima wana uwezo wa kufika katika  maonyesho asubuhi na kurudi jioni kwa kutumia usafiri wa miguu, baiskeli na gari na kuwa na mifano halisi ya kile kinachotakiwa katika shughuli zao katika eneo lao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,327FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles